Aliyekuwa RC Simiyu kizimbani shtaka la ulawiti

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:36 AM Jul 10 2024
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda (aliyevaa kofia),  akiongozwa na Makachelo wa Polisi, kuingia katika Mahakama ya Mkoa wa Mwanza jana, kabla ya kusomewa shtaka la kulawiti binti ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu mkoani Mwanza.
Picha: Vitus Audax
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda (aliyevaa kofia), akiongozwa na Makachelo wa Polisi, kuingia katika Mahakama ya Mkoa wa Mwanza jana, kabla ya kusomewa shtaka la kulawiti binti ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu mkoani Mwanza.

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Mwanza na kusomewa shtaka la kulawiti.

Kesi hiyo ya jinai namba 1883 ya mwaka 2024, ilifikishwa jana mahakamani huko mbele ya Hakimu Mfawidhi Mkuu Erick Marley.

 Upande wa Mashtaka unawakilishwa na Waendesha Mashtaka wa Serikali, Martha Mtiti na Magreth Mwaseba, Dk. Nawanda akidaiwa kutenda kosa hilo Juni 2 mwaka huu.

 Akisoma shtaka hilo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Magreth Mweseba alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu namba 154(1(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

 Kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu hicho kinaelekeza: "Mtu yeyote ambaye anamwingilia mtu yeyote kinyume cha maumbile, atakuwa ametenda kosa, na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha na wakati mwingine kifungo kisichopungua miaka 30."

 Mweseba alidai mahakamani huko kuwa mshtakiwa Dk. Nawanda, mkazi wa Nyamata, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, anashtakiwa kwa kosa la kumwingilia kinyume cha maumbile binti mwenye umri wa miaka 21 (jina tunahifadhi).

 Alidai kuwa Dk. Nawanda alitenda kosa hilo katika eneo la maegesho ya magari lililoko Rock City Mall, wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.

 Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa Dk. Nawanda alikana kutenda kosa hilo. Mwendesha Mashtaka Mwaseba alidaiwa mahakamani huko kuwa upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika, hivyo akaomba tarehe kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

 Wakili wa Utetezi wa Dk. Nawanda, Constantine Mutalemwa, aliomba mahakama hiyo kumwachia mteja wake kwa dhamana kwa kuwa kosa hilo linadhaminika.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Marley alisema dhamana iko wazi endapo mshtakiwa huyo akikidhi masharti ya kuwa na wadhamini wawili; mmoja awe mtumishi wa umma na mwingine wa sekta binafsi na raia wa Tanzania mwenye utambulisho rasmi pamoja na bondi ya mali isiyohamishika yenye thamani isiyopungua Sh. milioni tano.

Mshtakiwa huyo alitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana. Shauri hilo liliahirishwa hadi Julai 16 mwaka huu kwa ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali na kesi kuanza kusikilizwa.

Kabla ya kuahirisha shauri hilo, Hakimu Marley alisema dhamana hiyo itakoma endapo mshtakiwa atavunja sharti lolote la mahakama ikiwamo kutofika mahakamani.