ACT yataka serikali kuboresha msingi wa demokrasia

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:43 PM Sep 16 2024
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo akisikiliza kero za bodaboda kawe alipofika huko kwaajili ya mkutano wa hadhara.
Picha;Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo akisikiliza kero za bodaboda kawe alipofika huko kwaajili ya mkutano wa hadhara.

CHAMA Cha ACT Wazalendo kimeitaka serikali kuboresha msingi wa demokrasia kwa kuzingatia maazimio ya kikosi kazi ambayo yaliweka mikakati ya kuiponya nchi yetu.

Pia kimependekeza kurejeshwa upya mjadala wa katiba mpya ili kupata itakayo jali zaidi misingi ya demokrasia akikosoa kwamba iliyopo inampa mamlaka makubwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamesemwa leo na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara Isihaka Mchinjita alipozungumza na wananchi wa Kawe katika mkutano wa hadhara mkoani Dar es Salaam.

Amesema demokrasia ya nchi yetu kwa sasa ipo mikononi mwa Rais inategemea siku atakavyoamka akisisitiza hali hiyo inaakisi misingi ya utawala wa kikoloni.

"Kama tunazingatia demokrasi yetu ni muhimu tukaijengea misingi ya kisheria kuliko ya hisani ya Rais" amesema Mchinjita 

Katika mkutano huo ambao ni mwendelezo wa ziara za chama hicho zinazofanyika mikoa tofauti tofauti nchini alisema Kawe inakabiliwa na migogoro ya ardhi  akiitaka serikali kuangalia namna ya kuitatua.

Katika hilo, aliutaja mgogoro ule unaohusisha kiwanda cha saruji na wakazi maeneo ya Cha simba, chui, na tembo.

"Tunataka serikali ihakikishe maeneo hayo yanabaki kwa wananchi na  ipeleke mpango wa kurasimisha maeneo yao ili waishi kwa amani" alisema 

Amekemea kitendo cha baadhi ya aliowaita 'vigogo wa serikali' kugeuza Hifadhi ya Bahari Mbweni kwa kukata mikoko na kufanya makazi yao na kwamba kitendo hicho kinakinzana na mpango wa serikali wa kutunza mazingira.

"Wamekata mikoko hekari tano,  na Viongizo wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wakipigiwa simu na BMU ambao wamekabidhiwa jukumu la ulinzi wa fukwe wanagoma kutoa maelezo ya nini kimetokea" amesema Mchinjita 

Pia, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekosa mbinu mbadala ya kukabiliana na mafuriko Katika Kata ya Kawe ambao yamekuwa yakiathiri maeneo ya  Tegeta, Mbweni, Ununio, Boko, Bunju akisistiza hali hiyo imetokana na ubovu wa mipango miji iliyowekwa na serikali.

Kutokana na hali hiyo alishauri serikali iukate Misitu wa Mabwepande na igawe maeneo kwa wanachi ambao hukumbwa na mafuriko na wawezeshwe ujenzi Ili kuwakomboa na adha hiyo.

"Lengo letu kama chama cha upinzani tunataka serikali iliyoko madarakani  itafute suluhu ya makazi kwa wananchi wake. Pia iwajibike kwa kuwasaidia wananchi hao ambao msaada pekee wanaopewa na wakati wa mafuriko ni kuambiwa wamejenga bondeni.

"Viongozi wanapaswa kutafuta suluhu ya matatizo yanayowakabiri raia lakini yapo mambo ambayo ni kielezo cha wazi kwamba serikali ya CCM imeshindwa kuongoza taifa letu" amesema Mchinjita kwa ukali.

Amesema leo ukienda hospital za serikali jambo la kwanza  utakalokutana nalo ni uhaba wa wahudumu wa afya, madaktari, vifaa tiba, dawa na pamoja na upungufu huo bado gharama za matibabu ni kubwa.

Ameongeza kuwa katika hospital nyingi nchini Kuna historia za wananchi wanaoshindwa kupata matibabu kwa kutomudu gharama na wengine wanaokufa kutokana na sababu hiyo.

Akihitimisha mkutano wake aliwaomba Wanakawe kukiunga mkono chama hicho ili waweze kuja na mbinu mbadala za kutatua matatizo ya wananchi ambayo yameshindwa kutatuliwa na serikali ya CCM.