Rais Donald Trump aipa dunia siku 10

By Restuta James , Nipashe
Published at 05:55 PM Feb 20 2026
Rais wa Marekani, Donald Trump.
Picha: Mtandao
Rais wa Marekani, Donald Trump.

Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza siku 10 za kuamua hatima ya Iran, kama kutakuwa na makubaliano au mashambulizi ya kijeshi.

Akizungumza jana katika uzinduzi wa bodi yake ya Amani jijini Washington DC, Rais Trump alisema mazungumzo na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia lazima yafikie makubaliano yenye tija vinginevyo mambo mabaya yatatokea.

Katika siku za hivi karibuni, Marekani imeongeza vikosi vya kijeshi Ghuma ya Uajemi, huku ripoti zikieleza kuwa kuna hatua nzuri katika mazungumzo yanayoendelea nchini Uswisi.

Vyombo vya habari vya kimataifa ikiwamo BBC Verify imethibitisha picha zilizopigwa leo asubuhi Februari 20, 2026 na kuchapishwa kwenye X zinazoonyesha shehena ya ndege ya Marekani USS Gerald R Ford ikipitia Mlango-Bahari wa Gibraltar.

Picha hizo - zilizochukuliwa kutoka Gibraltar - zinaonyesha meli kubwa zaidi ya kivita duniani ikiwa inaelekea mashariki kutoka Atlantiki hadi Mediterania.

Pia BBC imethibitisha kwa kutumia ufuatiliaji wa meli kwamba moja ya meli katika kundi la meli za kubeba ndege za kivita za Ford, USS Mahan, ilipitia njia hiyo.

Rais Donald Trump ameitaka Iran kuafikiana kuhusu mpango wake wa nyuklia na kuonya kwamba vinginevyo “mambo mabaya yatatokea.”

BBC imetumia zana zinazopatikana hadharani za kufuatilia safari za ndege kama Flightradar24 ili kuangalia mienendo ya ndege za kijeshi za Marekani huku Washington ikiendelea kuimarisha vikosi vyake katika Mashariki ya Kati.

Picha ya skrini kutoka Flightradar24 imebaini ndege sita za kijeshi za Marekani zikiingia na kutoka Mashariki ya Kati leo Ijumaa.

Pamoja na safari za ndege za jeshi la anga pia nimeona ndege mbili za upelelezi za Jeshi la Wanamaji la Marekani P-8 Poseidon juu ya Mediterania - moja ikielekea magharibi kuelekea Gibraltar na nyingine nje ya pwani ya Crete.

Wakati huo huo, Waziri wa Mafuta wa Iran amesema "kila kitu kinawezekana" kuhusiana na uwezekano wa ushirikiano kati ya Tehran na Washington, katika nyanja za mafuta na gesi.

Hata hivyo, katika mahojiano na Shirika la Habari la ILNA, Mohsen Paknejad hakutaja muda wa kuanza kwa ushirikiano huo.

Hamid Ghanbari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya kiuchumi pia siku chache zilizopita alisema: "Maslahi ya pamoja katika nyanja za mafuta na gesi, nyanja za pamoja, uwekezaji wa madini na hata ununuzi wa ndege yamejumuishwa katika mazungumzo na Marekani."

Pia alisema kuwa Marekani haikunufaika kiuchumi katika makubaliano ya awali ya nyuklia, lakini "wakati huu, ili makubaliano hayo yawe endelevu, ni muhimu Marekani pia iweze kunufaika katika maeneo yenye faida kubwa na za haraka kiuchumi."

Chanzo: BBC