Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Libya ajiuzulu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:32 PM Apr 17 2024
Abdoulaye Bathily.
Picha: Yousef Murad/AP
Abdoulaye Bathily.

MJUMBE wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Abdoulaye Bathily amejiuzulu wadhifa wake, huku akisema kuwa shirika hilo la kimataifa haliwezi kufanikiwa kuunga mkono mabadiliko ya kisiasa ya nchi hiyo.

Bathily ambaye ni Waziri wa Zamani wa Senegal ameyasema hayo katika kikao na waandishi habari baada ya mkutano wa Baraza la Usalama ambapo ameelezea hali ilivyo mbaya katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, iliyokumbwa na mzozo na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya muongo mmoja.

Bathily amesema Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya - UNSMIL ulifanya juhudi nyingi chini ya uongozi wake katika kipindi cha miezi 18 iliyopita lakini hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na ukosefu wa dhamira ya kisiasa na nia njema kutoka kwa viongozi wa Libya, huku akisema kuwa hali hiyo ni ya kuhuzunisha kwa sababu idadi kubwa ya watu wa Libya wanatamani kuona mzozo huo ukimalizika.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekubali uamuzi wa kujiuzulu kwa Bathily na kumshukuru kwa juhudi zake za kurejesha amani na utulivu nchini Libya.