'Doria' ya Interpol mtandaoni yabaini ulaghai mkubwa Afrika

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:24 PM Feb 20 2026
'Doria' ya Interpol mtandaoni   yabaini ulaghai mkubwa Afrika
Picha:Mtandao
'Doria' ya Interpol mtandaoni yabaini ulaghai mkubwa Afrika

Shirika la Polisi wa kimataifa Interpol limesema vyombo vya kutekeleza sheria kutoka nchi 16 za Afrika vimefanikiwa kupata zaidi ya Dola za Marekani milioni 4.3 na kukamata watu 651, katika msako mkali dhidi ya ulaghai wa kimataifa wa mtandaoni.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano wiki hii, Interpol ilisema hatua hiyo iliyopewa jina la Operesheni Red Card 2.0 ilichukua muda wa wiki nane, kuanzia Desemba 8, 2025 hadi Januari 30, mwaka huu.

Baadhi ya nchi zilizoshiriki katika operesheni hiyo ni pamoja na Angola, Cameroon, Côte d'Ivoire, Kenya, Nigeria na Zimbabwe.

Ikizungumzia kesi maalum, taarifa ya shirika hilo ilionyesha kuwa polisi wa Nigeria walizuia njama za mtandao wa wahalifu za kuwalaghai watu kupitia miradi ya uwekezaji yenye mavuno mengi.

Walifuta zaidi ya akaunti 1,000 za ulaghai wa mitandao ya kijamii na kugundua jengo linalotumika kama msingi wa uhalifu huo.

Wakati huo huo, maafisa wa utekelezaji wa sheria wa Kenya na Ivory Coast walikamata mamia ya watu waliohusishwa na uwekezaji na miradi ya mikopo ya simu, wakikamata vifaa kadhaa vilivyotumika katika shughuli hizo haramu.

"Makundi haya ya uhalifu wa mtandao yanaleta madhara makubwa ya kifedha na kisaikolojia kwa watu binafsi, biashara na jumuiya nzima kwa ahadi zao za uongo," alisema Neal Jetton, Mkurugenzi wa Uhalifu wa shirika la Interpol.

Interpol ilisema ilichangia kwa kushirikisha wengine taarifa muhimu za kijasusi pamoja na ubadilishanaji habari kwa wakati halisi na mafunzo juu ya matumizi ya zana za uchunguzi wa kidijitali.

Kwa ujumla, operesheni hiyo ilifichua ulaghai unaohusishwa na hasara ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 45 na kubaini zaidi ya waathiriwa 1000, wengi wao kutoka Afrika.

BBC