Zaidi bil. 101/- zapokewa akaunti ya mirathi

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 01:02 PM Dec 11 2024
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.
Picha: Mtandao
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amesema katika miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, jumla Sh. bilioni 101.8 zilipokewa katika akaunti ya mirathi.

Kati yake, Sh. bilioni 77.8 zililipwa kwa warithi na Sh. bilioni 24 zinasubiri kulipwa.

Jaji Ibrahim alisema hayo jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka mitatu ya Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke tangu kuanzishwa mwaka 2021.

Alisema mirathi hubeba kiasi kikubwa cha fedha na uendeshaji wake unahitaji umakini na uadilifu wa hali ya juu vinginevyo inaweza kugubikwa na ubadhirifu.

Jaji Profesa Ibrahim alisema wakati wa kutayarisha Mpango Mkakati wa Mahakama na Programu ya Maboresho miaka ya 2014 hadi 2016, Mahakama ya Tanzania ilikuwa ikikabiliana na changamoto ya usimamizi wa fedha na mali za mirathi. 

Alisema kupitia mashauri ya mirathi Mahakama ilikuwa inalipa Sh. bilioni 3.8 kwa wasimamizi na warithi wa mirathi kiasi ambacho kinabeba uchumi mkubwa wa wananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. 

"Mahakama iliona ni muda mwafaka wa kuimarisha na kuboresha ushughulikiaji na usimamizi wa mashauri ya mirathi kwa kuyapa kipaumbele ili kuhakikisha wananchi na jamii kwa ujumla wanapata huduma na elimu ya usimamizi wa mirathi na utatuzi wa migogoro ya kifamilia ili kutumia muda wao zaidi katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo.

"Katika miaka ya fedha 2021/2022, 2022/2023, 2022/2024 na 2024/2025 jumla ya Sh. 101,876,509,671.81 zilipokewa kwenye akaunti ya mirathi, kati ya hizo jumla ya Sh. 77,846,349,370.59 zililipwa kwa warithi na jumla ya Sh. 24,030,169,397 zinasubiri kulipwa.

"Ipo changamoto kubwa ya baadhi ya wasimamizi wa mirathi kukiuka masharti ya kisheria juu ya majukumu yao ya usimamizi wa mirathi, baadhi ya wasimamizi hawaziishi ahadi walizoapishwa mahakamani," alisema Jaji Mkuu.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa, Kituo Jumuishi kimewahudumia wateja 580,610, kati ya hao 311,183 ni wanawake, 265,985 wanaume na 3,442 watoto.

Alitaja faida zilizopatikana katika kipindi cha miaka mitatu kuwa gharama zimepungua kwa wananchi na wadaiwa katika kufuatilia huduma za haki ambazo zinatolewa na wadau tofauti katika sehemu tofauti kwa kuwa utoaji wa huduma jumuishi unarahisisha huduma hizo kupatikana katika jengo moja.

"Kituo jumuishi cha masuala ya familia Temeke, kimebeba dhana ya maboresho kwa kuwa na mfumo wa utoaji haki ambao unalenga kuwafikishia huduma wananchi ambao ni wanyonge katika jamii na ambao huduma za kimahakama huwa haziwafikii kwa wepesi na kwa gharama nafuu. 

"Walengwa hapa ni wale katika jamii ambao huwa hawapati nafasi sawa na wengine katika kupata huduma za utoaji haki kwa mfano, wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu, wametajwa kuwa hawapati fursa sawa na wengine katika kufikia ngazi za utoaji haki," alisema.

Alisema katika kuhakikisha wananchi wenye kipato cha chini Dar es Salaam wanapata usafiri wa kuwafikisha katika Kituo Jumuishi Temeke, Andiko la Mradi wa Maboresho ya Mahakama iliitaka Mahakama ya Tanzania ifanye makubaliano na uongozi unaosimamia mabasi ya mwendokasi ili kuweka punguzo la nauli za mabasi yao kurahisisha usafiri wa wadaiwa wanaofuata huduma katika Kituo Jumuishi.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mwanabaraka Mnyukwa alisema: "Katika kipindi cha miaka mitatu tumekutana na changamoto ya ucheleweshaji wa kuhamisha mali kwenda kwa warithi, jamii kutokuwa na uelewa kuhusu usimamizi wa mirathi.

"Mahusiano wanandoa katika kuvunja ndoa na uelewa mdogo kuhusu kuandika wosia, kuandika wosia ifahamike kwamba si uchuro," alisema Jaji Mwanabaraka.

"Wanandoa wamekuwa na uadui, wanatakiwa kuwa na makubaliano katika haki ya kuwaona watoto na mgawanyo wa mali," alisema.

Alisema kituo kimehudumia idadi kubwa kwa miaka mitatu jumla ya watu 580,610 walihudumiwa wakiwamo wanawake 266,985, wanaume 311,183 na watoto 3442.

Jaji Mwanabaraka alisema jumla ya mashauri 22,929 yalisajiliwa kati ya hayo yaliyoamuliwa ni 20,077 na 852 hadi Agosti, mwaka huu yalikuwa hajasikilizwa.

Alisema migogoro inasababisha chuki kwa wanafamilia na kusababisha warithi kuchelewa kupata haki zao kwa wakati.