Washindi ubunifu mtandaoni waokota dodo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:25 AM Feb 16 2025
Matumizi ya Mtandao
PICHA:MTANDAO
Matumizi ya Mtandao

VIJANA wanne kati ya 697 wa shindano la wabunifu mtandaoni (Cyber-Champions 2025) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Intaneti Duniani, wamepata nafasi ya kufanya mafunzo kazini katika kituo cha utafiti na ubunifu kilichopo chini ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Vijana hao ni kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU) ambao walikuwa miongoni mwa wanafunzi 697 kutoka vyuo 43 walioshiriki.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha TEHAMA na kuchochea ubunifu wa teknolojia utakaosaidia ukuaji wa uchumi wa kidijiti.

Mkurugenzi wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari alisema watumiaji wa mtandao wameongezeka kwa asilimia 86 ndani ya miaka mitano.

Alisema katika maadhimisho ya Siku ya Intaneti Salama Zaidi Duniani (SID), Tanzania inaongoza Afrika na iko juu, na ya mfano duniani kwa usalama mitandaoni,na kwamba ya kwanza Afrika Mashariki na Kati, ya tatu Afrika ni miongoni mwa nchi 46 bora za mfano.

“SID inaadhimishwa kuhimiza matumizi salama na imara ya intaneti ikiwa ni pamoja na watumiaji na jamii kuepuka ulaghai mitandaoni. TCRA imeandaa shughuli mbalimbali Dodoma ikiwa ni pamoja na mkutano wa wadau,”alisema.

Awali akitangaza washindi hao, Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, Mhandisi Benedict Ndomba alisema wametoa zawadi hiyo ili kuhamasisha vijana kujihusisha na TEHAMA pamoja na kuchochea ubunifu wa teknolojia utakaosaidia ukuaji wa uchumi wa kidijiti.

Alisema shindano hilo wasichana walikuwa 95 na wavulana 602.

Fahirisi ya Usalama Mtandaoni Ulimwenguni (GCI) ya mwaka 2023 iliyotolewa Septemba 2024 inaonesha kwamba Tanzania imepanda viwango kwa pointi tisa kwenye nafasi yake Afrika na kwa pointi tatu Afrika Mashariki ndani ya miaka tisa, kati ya 2015 na 2024, na kwamba ilikuwa ya nne na 12 mtawalia mwaka 2015.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Bakari alisema kupaa kwa Tanzania kunatokana na

ufanisi katika kusimamia nguzo tano ya usalama mitandaoni, na kwamba ni sheria na ujenzi wa uwezo katika masuala ya usalama; mipango na mikakati ya kiufundi; mfumo wa usimamizi na uendeshaji pamoja na ushirikiano wa ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.