‘Wananchi lipeni kodi, tozo ili kurahisisha upatikanaji maendeleo’

By Neema Sawaka , Nipashe
Published at 06:53 AM Apr 17 2024
Mkurug Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, Khamis Katimba.
Picha: Maktaba
Mkurug Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, Khamis Katimba.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, Khamis Katimba amewataka wananchi kulipa tozo na kodi katika halmashauri hiyo ili kurahisisha upatikanaji maendeleo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Katimba alitoa wito huo wakati wa uzinduzi wa stendi mpya ya mabasi ya Isaka.
Alisema serikali inajitahidi kutekeleza malengo yake kama ilivyoahidi, hivyo wananchi nao wajitahidi kulipa tozo na kodi.
 
“Serikali ni ya wananchi, tunapaswa kulipa tozo za serikali na kujiepusha na utoroshaji au ukwepaji wa kulipa kodi kwa kuwa fedha zinazokusanywa hutumika kwa shughuli za maendeleo ya jamii ikiwemo ujenzi huu wa stendi,” alisema Katimba.
 
Alisema stendi hiyo ni moja ya mipango ya muda mrefu ya serikali na uzinduzi wake utaleta nafuu na kuongeza wigo wa kukuza uchumi wake na wa wananchi.
 
Alitoa wito kwa wananchi kuitumia ipasavyo stendi hiyo kwani uwepo wake ni moja ya sababu za ukuaji wa mji wa Isaka.
 
"Changamkieni viwanja kwani halmashauri imevipima karibu na stendi pembezoni mwa Barabara ya Isaka-Rwanda, pia stendi hii imelenga kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji itachangia halmashauri yetu kuongeza mapato kwa ajili ya kuhudumia wananchi kwani ni chanzo cha uhakika, " alisema. 
 
Alisema na timu yake ya wataalamu, wataendelea kuhakikisha mapato yanakusanywa na kutumika kama inavyoelekezwa na serikali.
 
Alisema hadi kufika Machi 31, mwaka huu, halmashauri hiyo  imekusanya asilimia 91 ya makusanyo ya Mfuko Mkuu ambayo ni sawa na  Shilingi bilioni 4.6.
 
Ofisa Mapato wa Halmashauri hiyo, Salehe Msosole, alishukuru uongozi wa halmashauri kwa kuweka msisitizo utendaji kazi uliotukuka kwa watumishi wake na kusaidia kuongeza mapato.
 
“Ukweli ulio wazi ni kuwa, ushirikiano wa Mwenyekiti wa Halmashauri, Mibako Mabubu na mkurugenzi wetu (Katimba) pamoja na watumishi umesaidia sana halmashauri hii hasa kuweka kipaumbele cha kwanza katika utendaji kazi wa kila siku,” alisema na kuongeza kuwa:
“Hiyo imesababisha usimamizi mzuri wa mapato hasa msisitizo wa kila diwani katika eneo lake huhakikisha tozo za serikali zinalipwa kama inavyotakiwa.”
 
Alisema Mkurugenzi huyo aliunda kikosi kazi kufanya doria usiku na mchana kuhakikisha wanadhibiti utoroshaji wa mapato.
 
“Tangu waanze usimamizi huu kila siku wanakamata magari yasiyopungua manne na Bajaj mbili,” alisema na kutoa wito kwa wafanyabiashara kulipa tozo za halmashauri kwa hiyari ili kujenga uchumi wa nchi na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan .
 
Diwani wa Kata ya Isaka,  Majuto Pazi, aliwaomba wananchi  kutumia fursa hiyo kujiongezea kipato.