Mradi wa REGROW wainua kiuchumi wanawake vijijini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:11 AM Apr 30 2024
Picha ikionesha taswira ya kupanda kwa uchumi.
Picha: Maktaba
Picha ikionesha taswira ya kupanda kwa uchumi.

SERIKALI inaendelea kuwainua kiuchumi Watanzania hususani wanawake waishio vijijini kupitia miradi mbalimbali ukiwemo wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

Mradi huo ambao unatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuendeleza utalii Kusini mwa Tanzania, umewainua kiuchumi wanawake kutoka vijiji vinanvyopakana na Hifadhi ya ya Ruaha, Udzungwa, Mikumi na Nyerere.

Wakizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, wanawake walionufaika na mradi huo kutoka katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hizo walisema kwa sasa maisha yao yameimarika kwani wameweza kuanzisha biashara zinazo wapatia kipato cha uhakika.

Mwamvita James kutoka Kijiji cha Madibira Mkoa wa Mbeya, alisema kabla ya mradi maisha yake yalikuwa ya kugangaiza  lakini kwa sasa anavuna magunia zaidi ya mia moja.

Alisema hali hiyo imemsaidia kujenga nyumba, kufungua biashara ya ushonaji iliyotoa ajira kwa wengine, huku akitoa wito kwa watu wengineo kutumia fursa zinazojitokeza katika maeneo yao.

Katibu wa kikundi cha Kordun kutoka jamii ya wamasai katika Kijiji cha Tungamalenga, Janeth Matambile alisema fedha walizopatiwa zimewasaidia kukopeshana na kuendeleza miradi mbalimbali waliyoianzisha ikiwemo unenepeshaji wa ng’ombe.

“Tulipatiwa fedha mbegu ambazo zimetusaidia kujenga mabanda ya ng’ombe ya kisasa kwa lengo la kuwanenepesha, mradi wa REGROW pia umetusaidia kuondokana na dhana potofu kuwa wanawake ni wa kukaa nyumbani tu na kwa sasa wanawake wanajishughulisha katika usindikaji wa maziwa na kutengeneza sanaa,” alisema Matambile.

Katibu Msaidizi wa kikundi cha Amani kilichopo Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, Upendo Vuliva alisema mradi ya REGROW umeimarisha upendo na furaha kwenye familia kwa kuwa inawawezesha wanawake kuchangia katika pato la familia.

Msimamizi wa mradi huo, Dk. Aenea Saanya alisema kwenye utekelezaji wa kipengele cha tatu, wanawake 127 kutoka kata ya Madibira na Miyombweni waliajiriwa katika mradi wa uboreshaji wa skimu ya umwagiliaji.

“Wanawake 10 kutoka vijiji vya Uturo, Gonakuvagogolo, Matebete, Chosi na Herman, Isele, Njombe, Mbuyuni, Makangalawe, Igumbilo/Isitu na Madibira wameajiriwa katika ujenzi unaondelea wa ofisi za Jumuiya za Watumia Maji,” alisema Dk. Saanya.

Dk. Saanya alisema hadi Februari mwaka huu mradi wa REGROW umewafikia wanawake 9,386 sawa na asilimia 56 ya wanufaika wote 16,872.

Kwa mujibu wa taarifa maalumu juu ya ushiriki wa wanawake katika mradi huo, hadi kufikia Februari 2024, mtaji wa vikundi vya COCOBA umekuwa ukiongezeka kwa wastani wa asilimia nne kwa mwezi kutoka Sh. milioni 61.3 Januari mwaka jana hadi Sh. bilioni 1.3 Januari mwaka huu huku idadi ya wanachama wanaostahili kupata mikopo kuongeza kutoka 483 hadi 3,496.

Aidha, wanawake 1,182 wameweza kuanzisha shughuli mpya za kujiongezea kipato, 1,814 wamewezeshwa kuboresha biashara au miradi yao na 1,859 wamewezeshwa kuboresha tija katika kilimo.

Aidha, katika uendeshaji wa mradi, asilimia 36 ya wafanyakazi ni wanawake ambao wapo katika taasisi zote.