Wahasibu Afrika waaswa kusimamia ukweli wa taaluma yao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:15 PM Dec 05 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko amewaasa wahasibu barani Afrika kuisimamia taaluma yao kikamilifu ili kuendeleza umuhimu na mchango na ukuaji wa uchumi duniani.

Ameyasema hayo jana Desemba 04, 2024 wakati akimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kufungaji Mkutano wa Pili wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Nchi za Afrika(AAAG) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

“Nataka niwaombe wahasibu mtambue kuwa taaluma yenu ni muhimu hata chochote kinachotokea katika sehemu zenu za kazi mtalaumiwa, hivyo mzuie hasara zinazoweza kutokea," alisema Dk. Biteko.

Aliwaasa  kusimamia taaluma yao kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma hata kama uamuzi wao unaweza kuwa na gharama“ Isimamieni taaluma yenu kwa wivu mkubwa na kusema ukweli hata kama mtachukiwa, mahali pa kazi ili kuwe na ufanisi ni muhimu kuwaheshimu wahasibu ili wakupe matokeo tarajiwa,”

Aidha, Dk. Biteko alisema ni muhimu kwa wahasibu hao kujiongezea ujuzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Pamoja na hayo alisema wahasibu wanatakiwa kuwa washauri wazuri wa viongozi wao ili waweze kufanya sahihi, huku akisema au inategemea wataalamu hao ili kuisaidia Afrika kunufaika na rasilimali zake.

“ AU inawategemea nyie wimbo wa Afrika ni tajiri utabaki kwenye vitabu kama hatutachukua hatua,” alisema Dk. Biteko.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande alimpongeza Mwenyekiti wa AAAG na Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Tanzania kwa kuandaa mkutano mzuri na kuwataka wahasibu kuwa na kuzingatia maadili ya kazi yao.

“Afrika tuna utajiri wa kuwa na watu wenye uwezo mkubwa katika kada hii ya uhasibu na ni imani yangu kupitia mkutano huu utaleta mabadiliko katika nchi zetu. 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Nchi za Afrika ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Lesotho, Malehlohonolo Mahase alisema Afrika inabadilika katika masula ya uhasibu, na kupitia mkutano huo wamepata fursa ya kubadilishana mawazo na ujuzi.

Alisema AAAG ni bodi ya Kiafrika inayolenga kwenda sambamba na Umoja wa Afrika huku ikisimamia nguzo za Umoja huo na kuwa mikataba inayoridhiwa na AU inatekelezwa pia na AAAG ili kuwa na ukuaji endelevu kwa nchi wanachama na Afrika kwa ujumla.

“ Kipaumbele chetu kimekuwa ni wahasibu wanavyoweza kusimamia masula ya uhasibu ikiwemo hazina za nchi zetu, tumezungumzia  kada ya uhasibu, kuimarisha mifumo yetu fedha na kushughulukia upotevu wa fedha katika nchi zetu,” alisema Mahase.

Mahase aliwataka Wahasibu Wakuu na Wahasibu Afrika kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika taaluma yao sambamba na kujiongezea ujuzi ili kuwa na ufanisi katika kazi zao.

Alitaja umuhimu wa wataalamu hao na kusema kuwa Afrika inawahitaji zaidi wakati huu ili kukusanya mapato na kuzuia njia zisizo halali za mianya ya fedha.

Akizungumzia baadhi ya maazio ya mkutako huo “ Mkutano huu umeazimia kuwa na matumizi bora ya rasilimali, kutumia mifumo ya kihasibu inayoshabihiana, kuwa mafunzo ya mara kwa mara kwa watu wa kada ya uhasibu,” 

Alisisitiza “ Kuongeza ushiriki wa wananchi kuhusu bajeti katika utekelezaji na utoaji taarifa ili kuongeza uwazi sambamba na kuwekeza kwenye masuala ya usalama mtandaoni,”

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Nchi za Afrika, Fredrick Riaga aliipongeza Tanzania kwa kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio makubwa.

Aliwashukuru Wahasibu Wakuu kutoka nchi mbalimbali walioshiriki akisema ni kiashiria cha kuimarisha sekta ya uhasibu Afrika ambapo washiriki 800 wametoka Tanzania huku mkutano wote ukiwa na idadi ya washiriki 1,000.

Alisema zaidi ya washiriki 1500 wamehudhuria mkutano huo kutoka nchi 26 barani Afrika.

Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Leonard Mkude aliwasihi washiriki wa mkutano huo kufanyia kazi yote waliyojifunza ili kuboresha kazi za uhasibu katika nchi zao.

Mkutano wa tatu wa AAAG umepangwa kufanyika nchini Ghana, Desemba mwaka 2025.