MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) itawapunguzia gharama za uhifadhi mizigo waathirika wa jengo lililoporomoka Kariakoo, jijini Dar es Salaam Novemba 16, mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, alitoa ahadi hiyo jana kwa waandishi wa habari na kueleza kwamba TPA ina utaratibu wa kuwapunguzia gharama za uhifadhi mizigo waathirika wa majanga ambao ni wateja wa bandari.
Alisema utaratibu wa kuwapa nafuu wadau waliopatwa na majanga pale wanapotoa taarifa zenye mashiko ni wa kawaida na imeshafanya hivyo mara kadhaa kwa utaratibu huu.
"Kuna janga na janga, lipo janga mtu ataondolewa na tozo ya asilimia 50, kuna majanga mengine kulingana na ukubwa, mdau anaweza kuondolewa tozo kabisa.
"Mfanyabiashara atatakiwa kutoa taarifa ya janga lililomkuta kwa wakala wake wa forodha na wakala atawasilisha taarifa hiyo TPA," alisema.
Alieleza kuwa kwa mantiki hiyo, wafanyabiashara na waathirika wa janga la Kariakoo wasiwasiliane na TPA moja kwa moja, bali wawasiliane na mawakala wao.
"Kwa utaratibu wetu tunahifadhi bure mzigo wa mfanyabiashara bandarini kwa siku tano tu baada ya hapo mfanyabiashara atatozwa kodi ya mzigo wake kulingana na siku mzigo huo utakapokaa bandarini," alifafanua.
Pia alisema kuwa TPA inawapa pole wafanyabiashara waliokutwa na tukio hilo, wakiwa kama wadau wakuu wa bandari hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa aliyopewa Rais Samia Suluhu Hassan siku ya Jumatano alipotembelea eneo hilo, watu 20 walikuwa wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa na kutibiwa katika hospitali mbalimbali jijini.
Sababu ya kuanguka kwa jengo hilo haijafahamika. Tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa maagizo ya Rais Samia, ameunda kamati maalumu kwa ajili ya ukaguzi wa majengo katika eneo hilo kuu la biashara ili kuepuka maafa katika siku za usoni.
Kamati hiyo pia inachunguza chanzo cha jengo hilo kuporomoka, kukiwa na dokezo kutoka kwa Rais Samia kuwa "hata kwa kuangalia kwa macho, nondo zilizotumika, na ubora wa kuta, vinaonesha ujenzi wa jengo hilo haukusimamiwa vizuri licha ya kupewa vibali na mamlaka husika".
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED