TIRA yakaa mguu sawa kupeleka elimu ya bima

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 07:49 AM Jun 26 2024
Nembo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
Picha: TIRA
Nembo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imesema imejipanga kuwafikia Watanzania wengi katika mikoa mbalimbali ili kuwaelimisha kuhusu masuala ya bima.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu – TIRA, Hawa Mniga, alisema wamejipanga kuhakikisha wanapita katika mikoa na maeneo mbalimbali kuhakikisha wananchi wanajua umuhimu wa bima lakini pia wanapata elimu. 

Alisema, TIRA imeendelea kutekeleza majukumu yake ikilenga kuwafikia Watanzania wengi kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha kuhusu masuala ya bima.

Alisema mbali na hilo pia walitoa elimu kuhusu umuhimu wa bima, ushauri wa kitaalamu na fursa ya kuwasilisha malalamiko yao kuhusu huduma za bima wanazopokea.

Ushiriki wa TIRA katika maadhimisho haya ya Wiki ya Utumishi wa Umma umekuwa wa manufaa makubwa na TIRA itaendelea kuhakikisha soko la bima nchini linabaki salama na lenye manufaa kwa watumiaji wote wa huduma za bima kwa kuendelea kutumia majukwaa mbalimbali kutoa elimu kuhusu bima.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kutokuwa wavivu wa kujifunza kuhusu bima, hivyo wanapopata wasaa wa elimu wanapaswa kuizingatia ili iwape manufaa hapo baadae.

Katika wiki ya utumishi wa umma iliomalizika hivi karibuni jijini Dodoma TIRA ilitoa elimu kwa watu waliohudhuria katika banda lao la maonyesho ya utumishi kwenye wiki hiyo.