Serikali yajizatiti kuboresha kilimo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:34 AM Feb 16 2025
Serikali  imejizatiti kuboresha sekta ya kilimo
PICHA:MTANDAO
Serikali imejizatiti kuboresha sekta ya kilimo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema serikali imejizatiti kuboresha na kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuandaa mipango yenye lengo la kuongeza fursa kwa wakulima.

Dk. Biteko alisema hayo juzi New Delhi, India  wakati akishiriki mkutano kuhusu masuala ya mazao jamii ya mikunde.

“Tunaongeza uwekezaji katika utafiti na kuboresha upatikanaji wa teknolojia za kisasa za kilimo. Kila  ofisa wa ugani nchini amepewa vifaa vyote muhimu ikiwamo pikipiki na kompyuta ili kutoa huduma nzuri na kwa wakati kwa wakulima wetu.,  alisema.

Pia alisema serikali imeboresha shughuli za usafirishaji wa bidhaa ikiwa ni pamoja na kurahisisha michakato ya uuzaji mazao.

 "Tanzania inaendeleza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo itaimarisha usafirishaji wa bidhaa yenye urefu wa takribani kilomita 500 kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo imekamilika na inatumika,” alisema. 

Biteko alisema kupitia mradi wa BBT (Building a Better Tomorrow) serikali imewezesha vijana kwa kuwapa ardhi, fedha na upatikanaji wa masoko sambamba na kuongeza huduma za kifedha za kidijitali.

Aidha, Dk. Biteko alisema India ni soko muhimu kwa mazao jamii ya kunde kutoka Tanzania na nchi inaweza kupata mafanikio makubwa zaidi. 

“Leo (juzi) nawaalika wawekezaji kutoka India na nchi zingine duniani kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo ya Tanzania kuanzia uzalishaji wa kisasa wa soya hadi uwekezaji katika mifumo ya usimamizi wa mavuno,” alisema.

Kuhusu maendeleo ya mazao jamii ya mikunde, alisema kuwa mwaka 2023, Tanzania ilizalisha takriban tani 250,000 za mbaazi ikiwa ni ongezeko la asilimia 56 ikilinganishwa na mwaka 2018.

Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 Tanzania itakuwa na ukuaji mkubwa katika pato la taifa kupitia kilimo. Maharage mekundu, mbaazi na choroko zinatarajiwa kufikia dola bilioni 1.47, dola milioni 84 na dola milioni 115. 

Aidha, ili kufikia uwezo huo, Tanzania imeweka mikakati ya kukuza sekta ya mazao jamii ya kunde kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa wakulima kusajiliwa, kuboresha mbinu za kilimo na teknolojia, kuhakikisha ubora na viwango vya mazao kulingana na mahitaji ya soko.

“Mazao jamii ya kunde nchini Tanzania yanauzwa kupitia mnada wa mtandaoni ambao unatoa fursa kwa wafanyabiashara kupata taarifa kuhusu mizigo iliyohifadhiwa katika ghala lililosajiliwa.

“Mfumo huu unahakikisha uwazi, ufuatiliaji na ufanisi katika biashara ya kimataifa. Mwaka 2024 pekee kupitia mfumo huu, wakulima wa Tanzania walipata zaidi ya dola milioni 91.31 kutoka katika biashara ya mbaazi, dengu na maharage ya soya, ubunifu huu si tu unaimarisha ushindani wetu bali pia unafungua fursa mpya za ushirikiano,” alisema.