MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameagiza kukamata mali za watu wanaodaiwa Sh. milioni 36 na Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambazo walizikusanya kama ushuru baada ya kupewa zabuni ya kukusanya mapato lakini hawakuzipeleka benki.
Alitoa agizo hilo jana kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) baada ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, kusema watu wanane akiwamo mtumishi mmoja wa serikali wanadaiwa zaidi ya Sh. milioni 37.
Dk. Mganga alisema wananchi saba ambao walipewa zabuni ya kukusanya ushuru wa halmashauri hiyo wanadaiwa Sh. milioni 32.5 wakati mtumishi aliyetajwa kwa jina la Dunstan Simpasa anadaiwa Sh.milioni 5.031.
Alisema mtumishi huyo kutokana na deni analodaiwa na halmashauri aliingia makubaliano na Benki ya NMB awe anakatwa Sh. 100,000 kila mwezi katika mshahara wake.
Alisema wananchi saba walikamatwa na polisi na baadaye wakaachiwa kwa dhamana lakini hakuna muda maalum uliowekwa kwa ajili ya kulipa fedha hizo.
Kutokana na hali hiyo, Dendego aliagiza ifikapo Machi 30, mwaka huu, fedha zote ziwe zimerejeshwa kwa asilimia 100 na ikishindikana, wadaiwa wote vitu vyao vikamatwe.
"Hawa watu wamechukua hela za serikali sasa sioni kama ni sawa kumfanya mtu arudishe hela anavyotaka yeye. Mimi naona si sawa na huyu mtumishi anayerudisha Sh. 100,000 kila mwezi atatumia miaka mitano kurudisha hela aliyoichukua akastarehe nayo lakini sisi tunachelewa kupeleka maendeleo kwa wananchi," alisema.
Dendego alisema katika jambo ambalo hapendi kuliona likijitokeza katika mkoa huu ni watu kuchukua hela za serikali na kuzifuja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED