WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ametangaza timu ya wataalamu ya kuandaa andiko maalum linalobeba maudhui ya Maono 2030 (Vision 2030) kwa sekta ya madini huku akiipa kibarua kizito cha kutilia mkazo maeneo nane yenye tija kwa Watanzania.
Akizungumza jana kwenye hafla ya kuzindua timu hiyo jijini hapa, Mavunde alisema timu hiyo itasaidia kuandaa ramani ya sekta ya madini kwa miaka michache ijayo ili ifikapo 2030, asilimia 50 ya eneo la Tanzania liwe limefanyiwa utafiti wa kina.
"Tunataka tuwaongoze vizuri watanzania kupitia sekta ya madini wakapate taarifa sahihi ya kilichomo chini ya ardhi ili kusaidia kukuza uchumi wetu, tukimaliza utafiti tutapata taarifa za Kijiolojia, ili wawekezaji waone maeneo ya kuwekeza," alisema.
Alisema dira hiyo ni mikakati ya wizara ilivyojipanga kutekeleza maono hayo yanayotokana na maelekezo ya Rais aliyoyatoa katika Mkoa wa Lindi ambapo alielekeza Wizara kuhakikisha inaboresha eneo la utafiti wa kina ili watanzania wasiendelee kuchimba kwa kubahatisha.
"Baada ya maelekezo ya Rais (Samia Suluhu Hassan), wizara tulikaa na kuja na 'Vision 2030 Madini ni Maisha na Utajiri', kwa nini 2030? Nchi yetu imejaliwa kuwa na madini ya aina mbalimbali lakini hatuna uwezo mkubwa wa kubaini kiwango cha madini tuliyo nayo chini ya ardhi. Tunataka mwaka 2030 tuwe tumefikia asilimia 50 ya eneo la Tanzania liwe limefanyiwa utafiti wa kina," alisema.
Alisema Tanzania ina ukubwa wa kilomita za mraba 945,000 na eneo lililofanyiwa utafiti wa kina wa Madini nchini ni asilimia 16.
"Katika eneo hili lililofanyiwa utafiti tumefanikiwa kwa Mwaka 2023/24 sekta ya madini imeongoza kwa mchango mkubwa wa kuiingizia nchi fedha za kigeni, asilimia 56 ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi, fedha zilizopatikana zinatokana na sekta hii ya madini, tulifanya mauzo ya bidhaa nje ya nchi zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.1," alisema.
Alibainisha kuwa timu hiyo itakabidhiwa hadidu za rejea 14 zitakazowaongoza kuandaa ramani ya utekelezaji wa maono hayo.
"Timu hii inayoongozwa na Prof. Mruma tumekabidhi sekta hii mikononi mwenu, mna nafasi ya kuleta mageuzi chanya au kuifanya Tanzania ipotee kwenye ramani, mna nafasi ya kutuonesha sekta hii ya madini na mchango wake ili watanzania wanufaike na rasilimali hii ambayo tumejaliwa," alisema.
Alitaja maeneo ya kuzingatiwa kwenye uandaaji wa andiko hilo ni mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa unaongezeka, upatikanaji wa fedha za kigeni, maendeleo ya viwanda na sekta mbalimbali, ushiriki wa watanzania kwenye sekta ya madini.
"Shirika letu la madini (STAMICO) tunataka kulifanya liwe shirika kiongozi. Nataka watu waje waombe kazi ya kuchoronga kwenye migodi yake na sio kwenda kuomba kazi ya kuchoronga kwenye migodi ya watu," alisema.
Pia alisema anatarajia andiko hilo litakuwa mwarobaini wa migogoro ya wachimbaji wakubwa na wadogo na kuvutia uwekezaji nchini.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Kamishna wa Madini, Dk. Abdulrahman Mwanga, alisema watahakikisha wanasimamia maono hayo ili kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk. David Mathayo, alipongeza wizara kwa hatua hiyo kwa kuwa ni mwarobaini wa kukuza uchumi wa nchi kupitia madini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED