MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema viwanja vya ndege ni sehemu muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, inategemea zaidi shughuli za utalii ambazo zinakwenda sambamba na uwepo wa miundombinu mizuri ya viwanja hivyo.
Aliyasema hayo jana visiwani Zanzibar alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi mbalimbali inayojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar.
Hemed alisema viwanja vya ndege ni milango mikuu ya nchi yoyote duniani inayotumika kwa kusafirishia wageni ambao huchangia kwa kiwango kikubwa kukua kwa uchumi na kuongezeka kwa pato la nchi husika.
Alisema utakapokamilika ujenzi wa miradi ya viwanja vya ndege vya jengo la kwanza na la pilli la abiria na eneo la biashara itaondoa changamoto ya msongamano wa abiria wanaokaa muda mrefu kusubiri kuhudumiwa.
Alisema pia itaongeza uwezo wa kutoa huduma bora na za haraka jambo ambalo litapelekea wageni wengi kuendelea kuitembelea Zanzibar mara kwa mara.
Hivyo, alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar kuhakikisha kila penye uwezekano wa kupatikana kwa kodi kuhakikisha kodi hiyo inakusanywa na kuingia serikalini ili kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Zanzibar.
Aidha, alisema serikali itaendelea kutoa ushirikano kwa kampuni zote zinazojenga miradi nchini ikiwemo kampuni ya Estim Constraction inayojenga miradi ya viwanja vya ndege vya Zanzibar, ili kuhakikisha wanakabidhi miradi hiyo kwa wakati uliopangwa na kwa kuzingatia viwango na ubora.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dk. Khalid Salum Muhammed alisema uchumi wa Zanzibar unategemea zaidi utalii, hivyo ni lazima kuimarisha miundombinu ya kimkakati ikiwemo viwanja vya ndege ili kuhakikisha utalii unakuwa kwa kasi zaidi na pato la nchi linaongezeka kupitia wageni wanaoingia Zanzibar.
Alisema ujenzi wa miradi hiyo inaendelea vizuri na hakuna changamoto yoyote hadi sasa ambayo itasababisha kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa miradi hiyo.
Aliahidi kuwa uongozi wa wizara utahakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa kiwango kilichokusidiwa ili kufikia malengo ya serikali iliyojiwekea.
Mshauri elekezi kutoka kampuni ya Anova Consult, Ibrahim Gasper alisema hadi sasa miradi yote inakwenda vizuri na ipo ndani ya wakati.
Hivyo, alimhakikishia Makamu wa Pili wa Rais kuwa watakabidhi miradi hiyo ndani ya muda uliopangwa na kwa kuzingatia viwango vya hali juu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED