Majaliwa ahimiza matumizi mifumo ya kielektroniki ukusanyaji mapato

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:51 AM Oct 06 2024
Majaliwa ahimiza matumizi mifumo ya kielektroniki ukusanyaji mapato.
Picha:Mtandao
Majaliwa ahimiza matumizi mifumo ya kielektroniki ukusanyaji mapato.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka maofisa masuhuli katika halmashauri zote nchini waweke msisitizo wa kutumia mifumo ya kielektroniki katika makusanyo badala ya kukusanya kwa fedha taslimu.

Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza mapato katika maeneo yao na kuepuka vishawishi vya kutumia vibaya fedha za umma ambazo zinakusanywa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

 Majaliwa aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.

“Suala la mapato ni lazima mliwekee msisitizo ili tupate matokeo mazuri katika halmashauri zetu,” alisema.

Majaliwa alitoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri kutumia mapato ya ndani katika kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka serikali kuu pekee.

Aliwataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu ili mipango na malengo ya serikali ya kuwahudumia Watanzania yaweze kutimia.

 Alisema watumishi wa umma ni wahudumu wa wananchi, hivyo wanapaswa kuwahudumia ipasavyo katika maeneo yao na kutatua kero zao.

“Sisi tunataka tuone mkifanya kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu usipofanya hivyo utakuwa unakosa sifa za kuwa mtumishi wa umma,” alisema.

Majaliwa aliwataka watumishi wa umma kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao kwa kuangalia hatua iliyofikiwa na sehemu iliyobaki, ili mpaka kufikia Juni mwakani miradi hiyo iwe imefikia zaidi ya asilimia 95 ya utekelezaji.

Kadhalika, aliwataka kusimamia maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na kutengeneza mazingira wezeshi ya kujiendeleza kiuchumi. 

“Punguzeni urasimu ili tujenge imani kwa tunao wahudumia, makundi yote yaliyo katika maeneo yenu yakiwamo ya vijana, wazee, wanawake na wenye ulemavu, lazima tuwafikie na kusimamia uchumi wao,” alisema.

Majaliwa ameweka jiwe la msingi la uzinduzi wa bweni na bwalo katika Shule ya Sekondari ya Kibasila iliyoko wilayani humo, uliogharimu Sh. bilioni 1.13.