Hoja tisa za TUCTA muswada wa mbadiliko ya sheria za kazi

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:40 AM Jan 18 2025
Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya.
Picha: Mtandao
Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya.

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limetoa hoja tisa kuhusu marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi kwa Mwaka 2024.

Moja ya hoja lilizotoa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, ni likizo ya dharura isiyo na malipo kwa mfanyakazi iwe angalau miaka mitano badala ya siku 30 zilizopendekezwa kwenye muswada.

Aidha, TUCTA imependekeza iwapo mama atajifungua mtoto njiti, apewe muda wa uangalizi wa mtoto mpaka mtoto akamilishe wiki 40 badala ya wiki 36 zilizopendekewa kisha mama apewe likizo ya uzazi ambayo haitaathiri muda wa uangalizi mtoto.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa baada ya kuwasilisha maoni kwa kamati hiyo, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alisema lengo la kuongezwa kwa muda wa likizo ya dharura ni kukidhi mahitaji ya mtu ambaye anakuwa kwenye mchakato wa kiuongozi au kimasomo.

Pia alisema muswada unapendekeza kuondoa neno ‘Sunday’ kwenye tafsiri inayohusu mshahara wa msingi na kwamba wao shirikisho linaona neno hilo libaki kwa sababu ni utamaduni wao wa muda mrefu,  hivyo kama kuna haja ya kuongeza neno jipya la ‘rest day’  basi liongezeke bila kuathiri neno ‘Sunday’.

 “Muswada pia unapendekeza kuongeza wigo wa tafsiri wa neno  ‘senior management employee’  kwa kujumuisha wafanyakazi wenye mamlaka ya kuajiri, kinidhamu na kusitisha ajira nao kutambulika kama ‘senior management employee’, TUCTA tumeshauri kamati maana ile ibaki kama ilivyokuwa kwa sababu wafanyakazi wengi watajikuta wanaangukia kwenye kada hiyo na kusababisha kukosa haki zao za msingi ikiwamo malipo ya saa ya ziada na kujumuika kupitia vyama vya wafanyakazi kama ilivyo katika sheria ya sasa,” alisema. 

Pia alisema TUCTA imependekeza kuwa mfanyakazi anayejiriwa kwa misingi ya kupata mafunzo afanye mafunzo hayo kwa kipindi cha miezi isiyozidi 12 tu kisha aajiriwe kama mfanyakazi kamili badala ya miezi 24 iliyopendekezwa katika  muswada.

 “Muswada unapendekeza kwenye masuala ya dharura/majanga mwajiri akae na mfanyakazi kukubaliana namna ya kushughulikia hilo suala. Maoni ya TUCTA ni kuwa pale ambapo kuna chama cha wafanyakazi mwajiri ashauriane na chama hicho ili kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi. Mfano hatima ya ajira na ujira kwa mfanyakazi,” alisema.  

Rais huyo alisema  TUCTA pia inashauri nafuu ya mtu anasitishiwa ajira kwa kutokufuata taratibu au kutokuwapo na sababu zenye mashiko basi alipwe fidia/nafuu ya mishahara kulingana na sheria iliyopo sasa tofauti na mapendekezo ya muswada ambayo yameweka ukomo wa mishahara isiyozidi miezi 12.

 “Mapendekezo ya muswada uliopo sasa yatasababisha uwepo wa fidia zisizo na uhalisia na pia kuwapa mamlaka waajiri kusitisha ajira za wafanyakazi pasipo kufuata utaratibu. 

 “Lakini pia itaondoa maana ya uwepo wa kanuni za utendaji bora tangazo la serikali namba 42 la mwaka 2007 TUCTA inashauri vyombo vyetu vya utatuzi wa migogoro ya kikazi nchini vimekuwa vikifanya kazi yake kwa umahiri mkubwa kwa kutoa fidia zinazostahiki kwa kuzingatia sheria iliyopo sasa,” alisema.

 Alisema TUCTA pia imependekeza kuwa wakati wa majadiliano ya mkataba wa hali bora za kazi katika taasisi za umma, endapo mkataba utapelekwa kwa Katibu Mkuu kwenye wizara husika, mkataba huo utolewe uamuzi na Katibu Mkuu kwenye wizara husika ndani ya siku 60 badala ya kutokuwa na ukomo wa muda wa kimaamuzi katika muswada wa sasa.

 Pamoja na hayo, alisema TUCTA imeendelea kupendekeza kuwa chama cha wafanyakazi chenye mamlaka ya kujadiliana na mwajiri wakati wa kuunda mabaraza ya wafanyakazi kiwe ni kile chama  kinachotambulika na mwajiri kama ilivyo kwenye sheria ya sasa na chama kilichosajiliwa na kina wanachama katika eneo hilo.