BODI ya Chai Tanzania (TBT), inatarajia kufufua mashamba ya chai yakiwamo ya Kilolo mkoani Iringa ili zao hilo liweze kuendelea kunufaisha wakulima na taifa kwa ujumla.
Kaimu Mkurugenzi wa bodi hiyo, Rukia Muwango, ambaye pia ni Meneja wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini, amesema hayo katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Chai Duniani.
Amesema, Tanzania inazalisha kilo milioni 112 za chai kwa mwaka, na kwamba inataka kuongeza uzalishaji huo kwa kufufua mashamba ya zao hilo ambayo kwa sasa hayatumiki.
"Bodi imedhamiria kuyerejesha mashamba ya chai ya serikali ambayo yametekelezwa kote nchini yakiwamo ya Kilolo, ikiwa ni moja ya mipango yetu ya kuimarisha kilimo cha zao la chai," amesema Rukia.
Amesema, serikali imekuwa mstari wa mbele kuimarisha kilimo huku zao la chai likiwa kati ya mazao ya biashara yenye nafasi kubwa katika kuchangia uchumi wa nchi.
"Bodi imejipanga kutumia vyema fursa zilizopo kwa kuendelea kufufua mashamba yote, lakini pia niwaombe Watanzania wapende kunywa chai kwa ajili ya kuimarisha afya zao," amesema.
Aidha, amesema ilianzisha mnada wa kwanaza wa chai wa Dar es Salaam, tangu Novemba 13 mwaka jana na imefanyika minada zaidi ya 10, lakini pia wameanzisha viwanda vidogo vya wakulima wadogo.
"Mfano wake ni kiwanda cha kusindika chai maalum (SAKARE) chini ya ufadhili wa Care International Tanzania, uanzishwaji wa mfumo wa kusajili na kutunza taarifa za wadau wa chai," anasema.
Ameongeza kuwa bodi imefanikiwa kukamilisha mkakati wa tasnia ya chai Tanzania, kuanzishwa kiwanda cha kuchakata chai maalum Kilolo ambacho kitakamilika mwezi ujao.
"Lakini pia katika jitihada za kuimarisha soko la chai, hivi karibuni bodi yetu na Wizara ya Kilimo tulikwenda nchi jirani kuangalia uwezekano wa kushiruikiana na taasisi nyingine zinazoshughulika na biashara ya chai kwa lengo la kukuza biashara yetu ya chai," amesema.
Ofisa Mkaguzi Bodi ya Chai Tanzania, Benjamin Nkonya amesema, kwa sasa soko la chai lina changamoto hasa kwenye maeneo ambayo imekuwa ikiuzwa kwa wingi.
"Soko kubwa la chai liko katika nchi za mashariki ya mbali na mashariki ya kati, lakini bahati mbaya baadhi ya nchi za maeneo hayo zimekumbwa na vita, kwa hiyo hata soko la chai lazima liyumbe," amesema Nkonya.
Amesema, pamoja na changamoto hizo za soko la chai kuyumba duniani, bado serikali inaendelea kujitahidi kuhakikisha chai inauzwa katika soko la Dar es Salaam na hata nje ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED