Balozi Hungary akunwa usimamizi wa Tanzania sera fedha, uchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:29 AM Oct 06 2024
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Hungary nchini, mwenye makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya, Zsolt Mészáros, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Dar es Salaam.
Picha:Mtandao
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Hungary nchini, mwenye makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya, Zsolt Mészáros, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Dar es Salaam.

BALOZI wa Hungary nchini mwenye makazi yake Nairobi, Kenya, Zsolt Mészáros, ameipongeza Tanzania kwa kusimamia vyema sera zake za fedha na uchumi, hatua iliyoifanya iendelee kuimarika kiuchumi.

Kutokana na hali hiyo, ameahidi kwamba nchi yake itaongeza ushirikiano kwa faida ya nchi hizo mbili.  

Mészáros aliyasema hayo jana katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba. 

Alisema nchi yake imekuwa ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania ikiwamo hatua kubwa inazochukua kuvutia uwekezaji wakiwamo wanaotoka nchini mwake.  

Balozi huyo aliahidi kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuchangia maendeleo hususan katika sekta za huduma za jamii kama vile maji kupitia mpango wake maalumu wa kushirikiana na serikali ujulikanao kama ‘Tied Aid Facility’. 

Waziri Nchemba alisema uchumi wa Tanzania umeimarika na katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2024/25,  umekua kwa wastani wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia tano katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita. 

Alisema makadirio ya ukuaji wa uchumi katika kipindi cha mwaka 2024/25 ni wastani wa asilimia 5.4 na asilimia 5.8 mtawalia kutokana na miongozo na usimamizi mzuri wa uchumi wa serikali.  

“Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Agosti,  mwaka huu, zinaonesha kuwa uchumi wetu umeimarika licha ya kuwapo kwa changamoto mbalimbali huku ukuaji huo ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na sekta za ujenzi, kilimo, fedha na sekta ya bima,” alisema Dk. Nchemba. 

Aidha, Dk. Nchemba alimweleza balozi huyo kuwa kasi ya mfumuko wa bei imedhibitiwa na kuwa katika kiwango cha asilimia 3.1 na kuwa katika wigo wa tarakimu moja. 

Alisema  kiwango kilichokubaliwa pia katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilizoweka ukomo wa asilimia nane na kiwango cha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) cha asilimia tatu hadi  saba.

Alisema uimara wa uchumi wa Tanzania umethibitishwa pia na mashirika yanayofanya tathimni ya hali ya uchumi wa nchi mbalimbali duniani ikiwamo Taasisi ya Moody’s ambayo hivi karibuni, iliipandisha daraja Tanzania kutoka Daraja B2 kwenda Daraja B1  na Taasisi ya Fitch ambayo imeipa Tanzania Daraja la B+ yenye Mtazamo Chanya. 

Dk. Nchemba alisema hatua hiyo imeifanya Tanzania na sekta binafsi kuaminiwa zaidi na taasisi za fedha za kimataifa kwamba zinaweza kuyafikia masoko ya fedha ya kimataifa na kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka maeneo mbalimbali duniani. 

Alitoa wito kwa wawekezaji kutoka Hungary kuwekeza nchini katika maeneo balimbali watakayoona yanawafaa kutokana na serikali kuweka mazingira bora yanayovutia uwekezaji.