Asilimia 80 wanafunzi UDOM wanasomeshwa na serikali

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 10:50 AM Dec 09 2024
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Lughano Kusiluka.
Picha: Mtandao
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Lughano Kusiluka.

ASILIMIA 80 ya wanafunzi wanaosoma Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wanafadhiliwa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Lughano Kusiluka, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini hapa kwenye mahafali ya 15 ya chuo hicho.

“Takribani asilimia 80 ya wanaosoma UDOM wanafadhiliwa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Kama ingetokea wanafunzi hawa hawajapata ufadhili idadi ya wanafunzi wanaohitimu chuoni hapa ingekuwa ndogo sana,” alisema.

Aidha, alisema hivi sasa UDOM imeanza kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali ikiwamo Pakstan ambapo kwa sasa kuna mwanafunzi mmoja. 

“Naomba niwatoe hofu kuwa elimu tunayoitoa UDOM ni ya viwango na wanafunzi wanaohitimu ambao wamepikwa na kuiva vizuri. Niwapongeze wakufunzi ambao mmekuwa mkisimamia misingi bora ya elimu kwa wanafunzi na kuhakikisha wanamaliza wakiwa na nidhamu,” alisema.

Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala, alisema baraza hilo limeendelea kuisimamia mikakati na sera ili kuhakikisha taaluma ya chuo inaendelea kukua. 

"Nawapongeza wahitimu waliomaliza masomo yao UDOM. Naipongeza serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya chuo," alisema.

Mmoja wa wahitimu wa Shahada ya Ualimu, Daud Mapelele aliipongeza serikali kwa namna ambavyo imeweka mazingira wezeshi kwa wahitimu kujiajiri pindi wanapohitimu elimu ya chuo ili kuepuka utegemezi.

Alisema (yeye) baada ya kumaliza elimu ya chuo kikuu alijiunga na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na kupata elimu ya ufundi umeme na kwa sasa amejiajiri na kuajiri wenzake wanne na  wote wanapata kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku.