WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameipa klabu ya Simba ‘mtihani’ wa kuhakikisha inatwaa ubingwa wa kombe la Shirikisho barani Afrika mwaka huu.
Waziri Mkuu alisema klabu hiyo ina nafasi ya kufanya hivyo kama itapambana zaidi kuanzia hapo ilipo sasa kuelekea kwenye hatua za juu zaidi katika michuano hiyo.
Aidha, amesema uwanja wa michezo jijini Arusha, ambao utatumika kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), umefikia asilimia 26.
Waziri Mkuu, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana, alipokuwa akitoa hotuba ya kuliahirisha Bunge.
“Ninaipongeza sana Simba Sports Club kwa kuingia hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho. Ninaitakia kila la heri na mafanikio katika hatua inayofuata. Watanzania tunalisubiri kwa hamu kombe la Ubingwa wa Shirikisho Afrika,” alisema.
Aidha, aliipongeza klabu ya Yanga kwa kuendelea kuwapa Watanzania burudani kupitia kandanda.
“Kadhalika, ninawapongeza wanachama na mashabiki wote wa timu hiyo kwa kutimiza miaka 90 tangu kuanzishwa kwake,” alisema.
Kuhusu maandalizi ya CHAN na yale ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), alisema mbali ya kujenga viwanja, Serikali itaandaa timu, hamasa kwa umma na kujitangaza kwenye masoko ya Utalii.
Majaliwa alisema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye sekta ya michezo ili iwe na tija kwa vijana na taifa kwa ujumla.
Alisema makubaliano kati ya serikali na kampuni ya Limonta S.P.A ya nchini Italia juzi, kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu jijini Dodoma, ni sehemu ya maandalizi hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwapongeza wanamichezo walioshiriki katika mashindano mbalimbali kitaifa na kimataifa na kuliletea Taifa heshima, wakiwamo wanariadha, mabondia na klabu za mpira wa miguu.
Tayari timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), imeshafuzu kushiriki michuano ya AFCON U17. Kadhalika, Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heros), imefuzu kushiriki michuano ya AFCON U20.
Timu ya Wanawake (Twiga Stars) nayo imefuzu kushiriki michuano ya Wanawake ya Afrika (WAFCON) na Taifa Stars, imefuzu kushiriki CHAN na AFCON 2025, mwaka huu.
Januari 14, mwaka huu, Shirikisho la Soka Barani Afrika lilitangaza kuahirisha michuano ya CHAN iliyokuwa imepangwa kufanyika mwezi huu, na kuisogeza mbele hadi Agosti 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED