Waziri aagiza kufanywa tathimini ujenzi uwanja wa AFCON Arusha

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 07:49 AM Feb 16 2025
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo Hamis Mwinjuma
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo Hamis Mwinjuma

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo Hamis Mwinjuma amewaagiza wataalamu kutoka wizara hiyo kufanya tathmini kuhusu ujenzi wa uwanja wa mazoezi kwaajili ya mashindano ya AFCON katika eneo la FFU, Morombo Jijini Arusha.

Waziri Mwinjuma ametoa maagizo hayo  Februari, 15, 2025 wakati akizindua michuano ya Soka ya Chuga Cup 2025 baada ya ombi la Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mrisho Gambo kuomba eneo hilo ujengwe uwanja wa kisasa kwaajili ya mazoezi wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa Barani Afrika AFCON 2027 ambayo Tanzania ni miongoni mwa nchi mwenyeji.

"Wananchi wa  Arusha wanayo kila sababu ya kuendelea kumwamini  mbunge wao Gambo kwa sababu amekuwa akipigania miradi mbalimbali ya wananchi jijini humo ikiwemo wazo la kujenga uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu tangu akiwa mkuu wa mkoa," amesema.

Aidha, ameeleza kiwa hajawahi kushuhudia kiongozi wa nchi  akiungwa mkono na wananchi wa Arusha kama ilivyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwinjuma amesema kutokana na miradi ya maendeleo inayopelekwa na serikali Jijini Arusha ndiyo sababu ya wao kuelekeza mapenzi juu yake.