Ziara ya Nchimbi yazoa 400 upinzani

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 08:31 AM Jun 09 2024
news
Picha: Romana Mallya
Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

ZAIDI ya wanachama 400 wakiwamo waliokuwa wagombea ubunge, madiwani na wenyeviti wa wilaya kutoka vyama vya upinzani, kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wametangaza kujiengua na kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wanachama hao wametangaza kuhamia CCM wakati wa ziara ya Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, iliyohusisha mikoa mitano ya Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga iliyomalizika jana.

Katika Jimbo la Korogwe Mjini, aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF) mwaka 2020, Amina Magogo, wenyeviti na madiwani tisa wametangaza kuhamia CCM pamoja na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama cha ADA TADEA  Singida.

Korogwe pekee, wanachama waliotangaza kujiunga chama tawala ni 225, akiwamo Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Korogwe, Nurdin Abubakar.

Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara siku moja kabla ya kuhitimisha ziara yake katika mikoa hiyo, Balozi Nchimbi alisema kazi za Rais Samia Suluhu Hassan ndizo zinazovutia wengi kurejea CCM.

Balozi Nchimbi alisema ziara aliyofanya katika mikoa hiyo imewezesha kuvuna wanachama hao kutoka upinzani kujiunga na chama tawala.

“Tunawashukuru ndugu zetu hawa ambao wameamua kwa hiari yao kujiunga na Chama Cha Mapinduzi na kwa kweli wameingia kwa kishindo maana si kwa wingi huu,” alisema.

Awali, akizungumza kwa niaba ya wenzake, Magogo alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuona juhudi zinazofanywa na Rais Samia, hivyo kumridhisha na kumwahidi Katibu Mkuu CCM kuendelea kuvuna wanachama wengine.

Akihutubia wananchi, Balozi Nchimbi alisema katika miaka mitatu ya Rais Samia, yamefanyika mambo makubwa ambayo hayajawahi kutokea.

Alisisitiza kwamba ziara hiyo wameifanya kwa ajili ya kuangalia uhai wa chama, kuangalia utekelezaji wa ilani na kusikiliza kero mbalimbali na mpaka sasa tangu  wameanza huo ni mkoa wa 10.

Aidha, alisema jambo linalotia faraja ni taarifa za utekelezaji wa ilani, mabadiliko waliyoona katika miradi ya elimu, afya, barabara na maji ambayo yamefanyika katika kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu historia ya nchi.

“Kwa miaka mitatu mambo yaliyofanyika hayajatokea na hii ni heshima kubwa kwa wanawake, Rais Samia amewapa heshima kubwa wanawake si tu wanawake wa Tanzania bali wanawake wa dunia nzima, hofu na mashaka ya watu siku zote kwamba wanawake hawawezi imekwisha.

“Tumejiridhisha pasi shaka kwamba, mwanamke ukimpa nafasi anatumia uwezo anaotumia kama kwenye familia anakuwa mama wa taifa, ndio maana Rais wetu amekuwa akisimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ambao umeongezeka mara dufu tangu amekuwa Rais,” alisema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, alisema upinzani hawaaminiki wamekuwa watu wa kuzua mambo na uchochezi na hivyo kuwatofautisha kati ya CCM na vyama vya upinzani.

"Ukiwauliza tunakwenda katika uchaguzi utawaambia nini wananchi ili wawaamini wanasema wanayo mambo matatu, ajenda yao ya kwanza watakwambia, 'katika mambo tuliyofanya vizuri nchi nzima tumekuwa na mpango kazi wa kufanyika maandamano' maandamano yanaleta maendeleo? Yametatua kero? " alihoji wananchi.

Makalla alisema itapasuka wakati wowote ndiyo maana wanazua mambo ili kuficha mgogoro uliopo.

"Mimi za ndani nilizonazo wakati wowote tutaanza kupokea viongozi wakubwa wa CHADEMA kwenda vyama vingine na wengine kuja Chama Cha Mapinduzi," alisema.