Idadi ya wanaojua kusoma yaongezeka nchini

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 03:52 PM Jun 23 2024
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiinyesha ripoti ya mafanikio kwenye sekta ya nishati.

KIWANGO cha kujua kusoma na kuandika kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea nchini kimeongezeka kwa asilimia 83.0 mwaka 2022 kutoka 78.1 2012.

Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu zitokanazo na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, ambazo zimeonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo mkoani Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa ripoti za Kidemografia, Kijamii, Kiuchumi na Mazingira zinazotokana na sensa ya watu na makazi ya 2022, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema ripoti hiyo pia imeonyesha mafanikio makubwa kwenye sekta ya nishati.

Amesema matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia yameongezeka ambako kaya zinazotumia umeme kwa ajili ya kupikia zimeongezeka kutoka asilimia 1.6 2012 hadi 4.3 2022 na Gesi kutoka asilimia 0.9 2012 hadi 9.4 2022.

"Idadi ya kaya zinazotumia kuni kwa ajili ya kupikia zimepungua kutoka asilimia 68.5 2012 hadi 55.5 2022. Haya ni mafanikio makubwa katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

"Sote tunafahamu kuhusu madhara yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni pamoja na kuchangia ongezeko la athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, afya za watumiaji pamoja na za kiuchumi katika jamii," amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa sekta ya maji na mazingira imeendelea kufanya vizuri ambako matokeo ya sensa yanaonesha kuwa asilimia 70.1 ya kaya zote zinatumia maji kutoka katika vyanzo vilivyoboreshwa. Kadhalika, asilimia 60.2 zinatumia vyoo vilivyoboreshwa. Akieleza kuwa hilo ni jambo la kujivunia kama taifa.