Imeelezwa kuwa tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa ni linaua watu wapatao Milioni Kumi kila mwaka huku nusu ya idadi ya vifo hivyo, vikiwa vinatokea barani Afrika.
Katika mkutano wao uliofanyika jijini Arusha, Tanzania, Mawaziri wa afya kutoka nchi tisa za Ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika wamefikia maazimio kwamba fedha na nyenzo Zaidi ziongezwa katika mapambano ya tatizo la usugu wa vielea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA).
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Afya ya Ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC), Profesa Yoswa Dambisya amesema kuwa tatizo la UVIDA linatarajiwa pia kuathiri Zaidi ya asilimia 3.5 ya pato la kila taifa ifikapo mwaka 2050.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amebainisha kuwa tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa kwa sasa linasababisha wagonjwa kutumia siku nyingi hospitalini wakati wakipatiwa tiba, kwa sababu ni vigumu sana kuyatibu magonjwa ambayo hayasikii dawa.
“Hivyo utaona kuwa, gharama za matibabu zinakuwa juu na pale ambapo dawa zitashindwa kabisa kufanya kazi, basi vifo hutokea,” alisema Mwalimu.
Inadaiwa kuwa zaidi ya watu Milioni 5 hufariki kila mwaka katika ukanda wa Afrika, Kusini mwa Sahara, kutokana na tatizo la UVIDA.
Hivi karibuni Tanzania ilizindua Kampeini dhidi ya matumizi mabaya ya dawa za tiba iitwayo ‘Holela-Holela Itakukosti,’ ambayo pia ilitambulishwa rasmi kwa viongozi na wataalamu wa afya kutoka nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika katika mkutano wao uliofanyika Jijini Arusha.
‘Holela Holela Itakukost,’ambayo inamaana ya "uzembe unagharimu," inaonyesha uhusiano muhimu kati ya afya ya binadamu, afya ya wanyama, na mazingira. Kwa kutumia mkakati wa sekta mtambuka, kampeni hii inalenga kushughulikia sababu mbalimbali za kijamii zinazopelekea tatizo la UVIDA na magonjwa ya zuonotiki na ilizinduliwa mwishoni mwa mwezi Mei 2024, ikiwa ni ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Makamu Rais (Mazingira), na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wa Breakthrough ACTION.
“Kampeni ya Holela Holela Itakukosti inaongozwa na balozi wake ‘KIDO,’ inatumia njia mbali mbali kuwafikia watu tofauti, wakiwemo viongozi katika jamii, viongozi wa dini, watoa huduma za afya, wananchi wa kawaida na hata watoto kupitia mbinu inayojumuisha sanaa na sayansi,” alisema Waziri Nyoni, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la John Hopkins Centre for Communications Program, ambao wanasimamia mradi wa Breakthrough Action.
"Tumeona pia umuhimu wa kuwaeleimisha wamiliki na watendaji wa maduka ya dawa, ili kuzuia ununuzi na uuzaji holela wa madawa makali ya tiba kwa wananchi bila kufuata maagizo ya daktari," alisema Nyoni.
Mawaziri na wawakilishi wa idara za afya kutoka nchi mbalimbali za ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika wameonesha nia ya kutumia kampeni ya Holela Holela Itakucost, kutoka Tanzania ili kusambaza elimu ya UVIDA katika nchi zao.
Mawaziri kutoka Lesotho na Uganda wao amesema tatizo kubwa la UVIDA katika nchi zao linawapata hasa wagonjwa wa kifua kikuu ambao huwa wanashindwa kutimiza tiba kwa kuacha matumizi ya dawa katikati, kutokana na umasikini.
“Dawa za Tiba ya kifua kikuu ni gharama, kwa hiyo unakuta wananchi wanashindwa kutimiza tiba yote na hivyo kusababisha vielea vya ugonjwa hua kujenga usugu dhidi ya maradhi,” walibainisha mawaziri hao.
Mawaziri wa afya wamekubaliana kuongeza nguvu zaidi katika kukabiliana na UVIDA, kupitia kampeni kama Holela-Holela ili kuhamasisha watu kupata na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kabla ya kutumia dawa, kutumia dozi ya dawa kikamilifu, na kufuata maelekezo ya wataalam wa mifugo au kilimo juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa mifugo na mimea.
Vita dhidi ya UVIDA ni moja ya maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa 14 wa Utendaji Bora pamoja na mkutano wa 30 wa Kamati ya Pamoja ya Ushauri ya Wakurugenzi (DJCC), ambapo kwa pamoja waliunga mkono na kupongeza kampeni hiyo na jitihada zake katika kupambana na UVIDA.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED