Wataalamu wa afya 450 kutibu Arusha bila malipo

By Beatrice Shayo , Nipashe Jumapili
Published at 02:31 PM Jun 23 2024
Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda.
Picha: Beatrice Shayo
Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda.

WATAALAMU wa afya 450 kutoka hospitali mbalimbali nchini na taasisi 40 wanatarajiwa kutoa matibabu na vipimo bila malipo kwa siku saba kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.

Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda, alibainisha hayo jana kuwa baada ya kukagua maandalizi ya kliniki hiyo ya afya inayotarajiwa kuzinduliwa kesho kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Alisema wataalamu hao, wakiwamo madakatari bingwa watatoa matitabu kwa wananchi bila gharama yoyote, hivyo ni muhimu wakajitokeza kwa wingi na kutibiwa.

"Ninaomba kuwakaribisha wananchi wote wa Arusha kujitokeza kwa wingi kwenye kliniki hiyo;  matibabu na dawa vitatolewa bure kwa kila mwananchi atakayebainika na kugundulika kuwa na magonjwa ya aina yoyote.
"Ndugu zangu asiwaambie mtu, kwenye suala la afya kuna watu wameuza nyumba zao, kuna watu wameuza viwanja, kuna watu wamefilisika biashara zao katika kupambana kuuguza ndugu zao na kuna nyakati ndugu zetu wameshindwa hata kukomboa miili ya ndugu zao kutokana na madeni ya gharama za matibabu.
 “Neema hii ambayo Mungu ametupa tukaitumie na mikono ya watumishi wa Mungu ikafungue baraka ili tukapate afya kupitia madaktari wetu hawa," alisema.

Makonda alizitaja hospitali na taasisi zitakazoshiriki kliniki hiyo na kutoa madaktari wake bingwa ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Hospitali ya Kanda KCMC, Hospitali ya Kanda Benjamin Mkapa, Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Mawenzi, SAIFEE na hospitali na taasisi zingine za ndani na nje ya Mkoa wa Arusha.