Watetezi Haki za Binadamu yawafunda wanafunzi vyuo vikuu

By Pilly Kigome , Nipashe Jumapili
Published at 10:06 PM Jun 23 2024
Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa
Picha: Mpigapicha Wetu
Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa

WANAFUNZI watakiwa kutobweteka kwa kuangalia masomo pekee bali wajikite na mambo ambayo yataleta tija katika jamii inayowazunguka.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa alipokuwa akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Asasi za Kibinadamu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Olengurumwa amewaasa wanafunzi hao kuachana na mambo ambayo hayana mchango katika elimu zao na badala yake wajikite katika yale yanayopanuwa wigo katika masomo yao ikiwemo kushiriki midahalo mbalimbali.

Amesema kwa sasa asilimia kubwa ya wanafunzi wamekuwa wakijikita katika mambo kama kushinda kwenye mitandao ya kijamii kufuatilia mambo yasiyo na tija.

“Acheni kulala, acheni kushinda kwenye vimbweta,kushinda kwenye mitandao ya kijamii pendeni makongamano na kujiunga kwenye vyama mbalimbali vya wanafunzi,” amesema Wakili Olengurumwa.

Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na madawati ya Vijana kutoka Asasi mbalimbali.

Francis Luziga kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora amewataka wanafunzi hao kujikita na masuala ya utetezi kwani itawajengea uwezo wa kujitetea na kuwatetea wenzao katika masuala mbalimbali ya kisheria endapo kutakuwa na kupinda kwa sheria.