Majaliwa ahamasisha wananchi kutumia fursa leo kujiandikisha

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:58 AM Oct 20 2024
Majaliwa ahamasisha wananchi kutumia fursa leo kujiandikisha.
Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu
Majaliwa ahamasisha wananchi kutumia fursa leo kujiandikisha.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amejiandikisha katika Daftari la Wakazi, kwa ajili ya uchaguzi viongozi wa Serikali za Mitaa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu na kuhamasisha ambao bado kutumia fursa iliyobaki leo (Jumapili).

Majaliwa ambaye alifuatana na mke wake, Mama Mary Majaliwa, alijiandikisha jana katika kituo cha kujiandikisha kilichoko Shule ya Msingi Nandagala iliyoko Kitongoji cha Nanguruwe, Ruangwa mkoani Lindi.

Akitoa taarifa ya uandikishaji, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Ruangwa, Frank Chonya, alisema wilaya hiyo ina tarafa tatu, kata 22, vijiji 90 na vitongoji 435 ambavyo vitahusika katika uchaguzi huo.

Chonya alisema wilaya hiyo imekadiria kuandikisha wakazi 123,803 na kati yao 60,188 ni wanaume na 63,615 wanawake.

Alisema hadi kufikia juzi, wameandikisha jumla ya watu 103,468 kati yao, wanaume ni 47,664 na wanawake ni 55,804.

 “Mchakato wa uandikishaji unaendelea hadi kesho (leo) saa 12 jioni,” alisema Chonya.

Akizungumza na wananchi waliokuwapo kituoni hapo, Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, aliwashukuru viongozi wa Serikali za Vijiji wa Kata ya Nandagala kwa kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha na kuifanya kata hiyo kuwa ya kwanza kwa uandikishaji katika jimbo hilo.

“Kazi ya uandikishaji inaendelea nchi nzima na mwisho wa uandikishaji ni kesho (leo). Tuwahimize wengine ambao bado hawajajiandikisha, nao pia waje kujiandikisha,” alisema Majaliwa.