Mwinyi ataka waumini kujitathmini kimatendo

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:27 AM Oct 20 2024
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha:Mtandao
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka waumini wa dini ya Kiislamu, kujitathmini na kujua umuhimu wa Ibada kwenye matendo yao ya kila siku.

Dk. Mwinyi alisema hayo alipotoa salamu kwa waumini hao, baada kujumuika nao kwenye ibada ya sala ya Ijumaa, Msikiti wa Muhammad Ali, Kidongo Chekundu, mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema ni wajibu wa kila muumini kuitathmini nafsi yake na anaowaongoza, ili kubaini kiasi gani maisha yao yanalingana na ibada wanazozitekeleza kila siku.

Alisema kuna mambo mengi yanaendelea ndani ya jamii, kwa sababu ya watu kukosa ucha Mungu.

 Dk. Mwinyi alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na udhalilishaji, ubakaji na wizi.

 Aidha, aliwahimiza waumini hao kufanya ibada, kwa kuwa ndiyo sababu kuu ya kuumbwa kwao.

 Akitoa salamu, Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Muft wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, aliwasisitiza viongozi kuwa mfano bora kwa watu wanaowaongoza, kwa kutenda mambo mema.

 Sheikh Khalid aliwasisitiza vijana kuacha kushawishika na kujiunga na makundi maovu kwa kisingizio cha dini, badala yake kusimamisha sala kwa kuchunga wakati na nidhamu.