TCRA: Simu nyingi zilipigwa Julai

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 04:19 PM Oct 20 2024
Jengo la Mamlaka ya Mawalisliano Tanzania (TCRA).
Picha: Mtandao
Jengo la Mamlaka ya Mawalisliano Tanzania (TCRA).

RIPOTI ya Takwimu za Mawasiliano robo ya mwaka inayoishia Septemba 2024 iliyotolewa ijumaa iliyopita na Mamlaka ya Mawalisliano Tanzania (TCRA), imeonesha kuwa Julai 2024 ulikuwa mwezi wenye idadi ya dakika nyingi zaidi ikilinganishwa na miezi mingine ya robo ya mwaka huo.

Aidha, mwezi Julai jumla ya dakika 14,095,650,019 zilitumika ikiwa ni dakika 7,188,565,697 ndani ya mtandao na dakika 6,907,084,322 nje ya mtandao, ikilinganishwa na Agosti 13,692,776,501 na Septemba 13,333,450,458.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo takriban dakika bilioni 41.1 zilitumika katika robo mwaka iliyoishia Septemba 2024 ikilinganishwa na dakika bilioni 39.6 katika robo mwaka iliyoishia Juni 2024.

Aidha, imeonesha kuwa dakika nyingi za sauti nchini zilitumika kwenye simu za ndani ya mtandao sawa na asilimia 51.3 kuliko simu za nje ya mtandao asilimia 48.7.

“ Takwimu zinaonesha kuwa watu walipendelea zaidi kupiga simu ndani ya mtandao mmoja kuliko kupiga nje ya mtandao. Airtel imeongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya dakika za ndani ya mtandao kwa asilimia 38.8 na nje ya mtandao asilimia 30.5.

Pia idadi ya laini za mtu kwa mtu zilizosajiliwa imeongezeka kutoka milioni 76.6 hadi milioni 80.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia tano kwa miezi mitatu.

Ripoti hiyo ambayo imetolewa juzi na TCRA, imeonyesha pia ilani za simu za mkononi na mezani kwa kampuni tano za simu zimeongezeka kutoka milioni 75.6 hadi 79.6 sawa na asilimoa 5.4 katika kipindi hicho, ikiwa ni wastani wa asilimia 1.7.

Aidha, laini za mashine kwa mashine kwa kila mtoa huduma zimeongezeka kutoka 995,494 hadi milioni 1.02 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.8.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa Dar es Salaam ilishika nafasi ya kwanza kwa kuwa na laini milioni 14.8, Mwanza ilishika nafasi ya pili kwa kuwa na laini milioni 5.3, Arusha ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na laini milioni 4.9, Mbeya ilishika nafasi ya nne ikiwa na laini milioni 4.6, na Dodoma ilishika nafasi ya tano kwa kuwa na laini milioni 4.3.

Kwa upande wa Zanzibar mikoa yenye laini chache zilizosajiliwa katika robo ya kwanza ya 2024/2025 ni Kaskazini Unguja yenye laini 73,743, Kusini Unguja yenye laini 110,970, na Kusini Pemba yenye laini 124,472.