INEC yataja sababu za kuahirisha maboresho Daftari la Wapigakura

By Adela Madyane , Nipashe Jumapili
Published at 08:10 AM Jun 23 2024
Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele.
Picha: INEC
Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele.

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeeleza sababu ya kuahirisha maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapigakura hadi Julai 20 mwaka huu kuwa ni kuzingatia maoni ya wadau katika mikutano iliyofanyika Dar es Salaam na Kigoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kigoma, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele alisema awali uzinduzi ulipangwa kufanyika Julai Mosi, mwaka huu na baada ya kusogezwa mbele, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa atazindua.  

"Tume imezingatia maoni na ushauri wa wadau. Hivyo, zoezi la uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapigakura litaanza tarehe 20 hadi 26 Julai, 2024 badala ya tarehe Mosi hadi 7 Julai, 2024, mkoani Kigoma na uzinduzi utafanyika siku hiyo ya tarehe 20 Julai, 2024," alisema. 

Alifafanua kuwa tume ilifanya mikutano tisa ya wadau ngazi ya taifa mkoani Dar es Salaam kati ya Juni 7 hadi 15 mwaka huu na kwamba mkutano wa wadau ngazi ya Mkoa wa Kigoma ulifanyika Juni 19 mwaka huu. 

Aliwataja wadau waliokutana na tume ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wawakilishi wa asasi za kiraia, wahariri wa vyombo vya habari, waandishi wa habari, maofisa habari wa mikoa na halmashauri, wawakilishi wa makundi mbalimbali ya vijana, watu wenye ulemavu, wanawake na wazee wa kimila. 

"Vyama vya siasa vilitoa maoni na ushauri wa kupatiwa muda wa kutosha kwa ajili ya kupata mawakala wa uandikishaji ili mawakala hao waweze kushiriki katika zoezi kikamilifu.  

"Aidha, vyama vilishauri tume isogeze mbele muda wa kuanza kwa zoezi la uboreshaji ili kutoa fursa kwa wao kuhamasisha wananchi na wafuasi wao kujitokeza katika zoezi hilo,” alisema Jaji Mwambegele. 

Wengine ni taasisi na asasi zilizoomba kibali cha kutoa elimu ya mpigakura wakati wa uboreshaji ambazo zilieleza kuwa kibali kinapotolewa na tume huwa ni muda mfupi kufikia uboreshaji kuanza na wakashauri tume ione namna ya kutoa kibali kwa muda utakaowawezesha kupata fedha kutoka kwa wafadhili ili zoezi likianza nao waanze kutoa elimu hiyo. 

Maoni mengine ya wadau yaliyosababisha tume kufikia uamuzi huo wa kusogeza mbele tarehe ya kuanza na kuzindua uboreshaji daftari ni yale ya kuishauri tume ijipe muda wa kutosha kutoa elimu ya mpigakura kwa wadau na wananchi kabla ya kuanza kwa zoezi lenyewe, ili wananchi wengi waelewe zoezi husika na hivyo kuwawezesha kujitokeza kwa wingi wakati litakapoanza.