Tutasimamia ardhi ya wananchi Mafia iliyoporwa na mwekezaji inarejeshwa - Ado

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 02:59 PM Sep 15 2024
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu
Picha:Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu amewaeleza wananchi wa vijiji vya Kata za Ndagoni, Baleni na Kirongwe kwamba chama kitasimama nao ili kukabiliana na jaribio la kuporwa kwa ardhi na mwekezaji kwa msaada wa viongozi wa Wilaya ya Mafia.

Ametoa msimamo huo akiwa katika ziara kwenye jimbo la Mafia mkoani Pwani jana Septemba 14, 2024 mara baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kupitia viongozi wao juu ya kuwepo kwa hofu, wasiwasi na vitisho vya kuondolewa kwenye ardhi yao yenye ukubwa wa ekari 4092. 

“Tunafahamu hapa mafia kuna mgogoro wa ardhi, ardhi ni uhai, ardhi ni urithi wetu. Hapa mafia kwenye kisiwa kidogo hiki mtu akikupora ardhi, anakuwa ndio amekupora uhai wako. Watu wa mafia sisi, ACT Wazalendo tumetangaza vita dhidi ya wezi wa rasilimali zenu. Kwa hiyo, nanyi tunawaomba, msimame imara, mtuunge mkono katika mapambano haya. Mkiwa na tatizo lolote naomba mtueleze… tumejitoa mhanga, tutawapambania.” alisema Ado Shaibu.

Mnamo Mei 28, 2015 Serikali kupitia amri ya Rais ilibatilisha Hati ya haki ya kumiliki ardhi juu ya Shamba Na. 86 eneo la Utumaini iliyokuwa inamilikiwa na Fazal Bhaji Jessa Limited. Kupitia tangazo hilo wananchi walikuwa na matumaini ya kurejeshewa ardhi yao lakini hadi leo hawajarejeshewa na kuna watu wengine wanaojiita wawekezaji wanaendelea kulishikilia na kumega maeneo mengine ya wananchi.

Katibu mkuu huyo alisema viongozi wa Serikali wasipochukua hatua haraka za kurejesha ardhi ya wananchi chama cha ACT Wazalendo kitachukua hatua ya kwenda mahakamani kuhakikisha haki inatendeka kwa wanachi hao. 

Kwa upande mwingine, Ado alisema maeneo mengi ya Mkoa wa Pwani na sehemu zingine nchini ambayo yalifanyiwa maamuzi ya kubatilishwa hatimiliki ya mashamba yasiyoendelezwa ili kurejeshwa kwa wananchi bado utekelezaji wake hauridhishi. Jambo ambalo linaendeleza migogoro ya ardhi nchini.

Hivyo, alitoa wito kwa Serikali kuwa pamoja na uwekezaji ni muhimu lakini ugawaji wa ardhi kwa wawekezaji usiathiri haki na matumizi ya ardhi ya wakulima na wafugaji kwa sababu ardhi kwao ndio ajira, ndio elimu, ndio urithi, ndio uhai na ndio rasilimali pekee ya kuzalisha chakula kwa matumizi yao na Taifa kwa ujumla. Endapo haki na mahitaji ya ardhi kwa wazalishaji wadogo yatapewa kipaumbele ni dhahiri kuwa migogoro ya ardhi itaisha.

"ACT Wazalendo tunaamini suala la migogoro ya ardhi linapaswa kupewa uzito mkubwa katika mijadala ya kisera, maamuzi na uongozi. Tunaamini katika TAIFA LA WOTE, MASLAHI YA WOTE. Hivyo ardhi lazima iwe na manufaa kwa wote na sio Serikali au wawekezaji tu."