Tangi la gesi kujengwa Soko la Samaki Feri

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 12:20 PM Sep 15 2024
MBUNGE wa Jimbo la Ilala na Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu
Picha:Mauld Mmbaga
MBUNGE wa Jimbo la Ilala na Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu

MBUNGE wa Jimbo la Ilala na Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu amesema wamefikia makubaliano ya kisheria na kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tangi kubwa la kisasa la gesi ambalo litagharimu zaidi ya Sh. Milioni 300 katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa kuutambulisha mradi huo, Zungu amesema wafanyabiashara wa kukaanga samaki katika soko hilo wamekuwa wakipata hasara ya kununua mitungi ya gesi lakini ni asilimia 45 tu ndio inafanya kazi kutokana na mazingira ya gesi kuganda na kuwa barafu.

Amesema kutokana na  hasara hiyo wameona waje na mradi wa tengi la gesi la jumla ambalo kila mtu atakuwa na luku na matumizi yake hali itakayosaidia matumizi kuwa mazuri na ya gharama nafuu.

“Kikubwa tunaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu  Hassan katika kutunza mazingira yetu, moshi wa kuni na mkaa unaharibu mazingira katika nchi yetu, hivyo tunaungana na Rais pamoja na wadau wetu.

“Tunawashukuru  sana kampuni ya Oryx Gas ambayo imekubaliana kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kusaidia kundi hili la wafanyabiashara wa kukaanga  samaki wapate nishati safi na salama lakini kwa gharama ya fedha wanazotoa," amesema Zungu.

Ameongeza kuwa mpaka sasa hatua walizochukua kisheria zimekamilika

Kwa asilimia 90 na hayo yote wanayofanya ni maelekezo  ya Rais Samia kuwatazama wananchi wake na kuhakikisha kila mmoja anaendesha shughuli zake kwa gharama stahimilivu.

“Viongozi wote wa Halmashauri ya Ilala walifanya jitihada za kuhakikisha mchakato wa ujenzi wa tangi hilo unatekelezwa na walifanya jitihada za kufanikisha kupatikana kwa eneo la mradi huu ambao umekuja kwa maslahi mapana ya wafanyabiashara, mazingira na taifa kwa ujumla,” amesema Zungu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, Ashelly Mbasha.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, Ashelly Mbasha, amesema wanategemea kuuanza mapema iwezekanavyo utekelezaji wa mradi huo, huku wakiomba uhakika wa ulinzi wa miundombinu.

“Tunaweka miundombinu ya gharama kubwa kwa kuwa gesi inataka usalama mkubwa. Kwahiyo tunaomba ulinzi wa hii miundombinu ili iweze kutusaidia kwa niaba ya wafanyabiashara wote.

Amesema Oryx wataendelea kushirikiana na serikali huku wakimshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilala kwa ubunifu huo mkubwa ambao amekuja nao, utakaokwenda kusababisha soko kuwa safi na lenye usalama.

“Pia tunampongeza Rais Samia na kampeni yake hii ya kuhakikisha mpaka mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi. Tunaendelea kuwakaribisha wadau wengine wote kutoka kampuni binafsi, mashirika na taasisi tufanye kazi na kuhakikisha ajenda ya rais tunaifikisha pamoja,” amesema Mbasha.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omar Kumbilamoto, amesema jitihada hizo zinatokana na maelekezo kutoka kwa Rais Samia ya kuhakikisha wanabadilisha  matumizi ya kuni na mkaa na kuingia katika matumizi ya gesi katika soko hilo na Tanzania kwa ujumla.

“Niwaombe wafanyabiashara tupokee mabadiliko kwani tunajua mabadiliko yanachangamoto lakini natumaini watayakubali muda sio mrefu. Nawashukuru Oryx ambao wanakuja  kuleta msaada wa zaidi ya Sh. milioni 300,” amesema Kumbilamoto.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omar Kumbilamoto.