Wizara ya Madini yavunja rekodi ukusanyaji wa maduhuli

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:14 PM Sep 15 2024
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amepongeza maafisa madini wakazi wa mikoa kwa kuvunja rekodi ya kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 196 kwa kipindi cha miezi miwili katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kiasi ambacho ni zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 161 kilichokusanywa kwa mwaka mzima wa fedha 2015/2016.

Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Septemba 15, 2024 kupitia kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini ikiwa ni pamoja na  wakurugenzi, mameneja na maafisa madini wakazi wa mikoa chenye lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha Sekta ya Madini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia ukusanyaji wa maduhuli, udhibiti wa utoroshaji wa madini, udhibiti wa mianya ya upotevu wa makusanyo na kuimarisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

Wengine waliohudhuria katika kikao hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, Kamishna wa Madini, Dk. Abdulrahman Mwanga, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Buriani na Mkuu wa Wilaya ya Tanga,  Jafari Kubecha.

Amesema kuwa tangu kufanyika kwa maboresho ya Sheria na kanuni za Madini, kupitia Tume ya Madini, Wizara ya Madini imeendelea kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli kutoka mwaka hadi mwaka siri ikiwa ni ubunifu wa ukusanyaji wa maduhuli kwa kudhibiti mianya ya utoroshaji wa madini.

“Niwapongeze kwa kazi nzuri sana ya ukusanyaji wa maduhuli hasa katika kipindi za kuanzia mwezi Julai hadi sasa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 196 zimekusanywa, kiasi ambacho kinazidi kiasi kilichokusanywa kwa mwaka mzima wa fedha wa mwaka 2015/2016,” amesisitiza Mavunde.

Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya Madini kupitia uwekaji wa mazingira rafiki ya uwekezaji na kuongeza bajeti ya Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 hadi shilingi bilioni 231 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.

“Bajeti hii kubwa tuliyopewa inakwenda kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa kama vile magari 89 na pikipiki 140 ambazo zitatumika kuyafikia maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa madini na ukusanyaji wa maduhuli.

Aidha, Mavunde amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kusimamia Sekta ya Madini kwa kufuata Sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuwa wasisite kuchukua hatua za kisheria kwa haki pale sheria na taratibu zinazozimamia Sekta ya Madini zinapokiukwa.

Wakati huohuo amempongeza aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini,  Yahya Samamba kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na kuteuliwa kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na kuwataka watendaji wote kuendelea kumpa ushirikiano.

Ikiwa ni mkakati wa usimamizi bora wa Sekta ya Madini, Mavunde ametoa maagizo matano kwa maafisa madini wakazi wa mikoa ikiwa ni pamoja na utatuzi wa migogoro ya wachimbaji wa madini kwa haraka kwa kusimamia haki badala ya kusubiri kufika ngazi za juu, kuimarisha udhibiti wa utoroshaji wa madini kwa kushirikiana na vikosi kazi na vyombo vya ulinzi na usalama na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Burian.

Maagizo mengine ni pamoja na Ofisi ya Kamishna wa Madini kwa kushirikiana na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kushirikiana kwa pamoja kuwalea, kuwakuza na kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini na kuimarisha ushirikiano kati yao na watumishi na watendaji wengine wa Sekta ya Madini.

Wakati huohuo akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa amepongeza hatua ya Waziri Mavunde kuendeleza falsafa yake ya kushirikisha maono yake kwa watendaji wa Wizara na Taasisi hali iliyopelekea Sekta ya Madini kuendelea kufanya vizuri kwenye uchumi wa nchi.

“Kupitia  ushirikishwaji wa maono yako kwa watendaji wa Wizara ya Madini na Taasisi zake, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua ambapo tuna uhakika ifikapo mwaka 2025 utakuwa umefikia asilimia 10,” amesisitiza Dk. Kiruswa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Wizara na Taasisi zake ipo tayari kufanyia kazi maelekezo mazuri yanayoendelea kutolewa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na rasilimali za madini nchini.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Buriani mbali na kupongeza utendaji wa Waziri Mavunde amesema kuwa Sekta ya Madini imechangia kwa kiasi kikubwa cha ukusanyaji wa mapato ya mkoa na kualika wawekezaji kujitokeza kwenye uwekezaji katika mkoa huo hasa ikizingatiwa kuna wingi wa madini ya metali, ujenzi, vito na ya viwandani.

Pia ameomba wachimbaji wadogo wa madini na wakinamama wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini kusaidiwa kwa kupewa mitaji na elimu kuhusu uchimbaji wa madini.

4