Wizara: Maandalizi ya ujauzito huepusha mgongo wazi, vichwa vikubwa

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 12:54 PM Sep 15 2024
Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ahmad Makuwani (katikati), akizungumza siku ya mbio hizo.
PICHA: MTANDAO
Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ahmad Makuwani (katikati), akizungumza siku ya mbio hizo.

MKURUGENZI wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ahmad Makuwani, amesema katika dunia iliyokua katika teknolojia ya tiba na uchunguzi wa mapema ni muhimu.

Amesema, ni vyema wanawake wanaotarajia kupata watoto kubadaili mtazamo kwa kutobeba mimba bila kufanya uchunguzi na maandalizi kwa kutumia vidonge vya madini chuma.

Makuwani aliyasema hayo wakati Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), ikitekeleza mradi wa mbio ndefu, fupi na za kati.

Ikiwa ni msimu wa nne wa mbio hizo, lengo ni kusaidia matibabu ya watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi na kuzindua kampeni ya kuwafikia watoto wote wanaozaliwa na tatizo hilo nchini.

“Watoto wanaozaliwa na mgongo wazi na kichwa kikubwa kuna njia za kuepuka wale mabinti ambao wanaotarajia kushika ujauzito katika dunia iliyokua na teknolojia si vyema kufanya hivyo yaani kushika ujauzito kwa bahati mbaya. 

“Fika kwa wataalamu wakakishauri, wakupe na vidonge vya 'folic acid', ili kupunguza hatari ya kupata mtoto wa tatizo hilo. Au ukishashika ujauzito mwezi wa kwanza huo huo, fika katika vituo vyetu ukapata ushauri na ipewe dawa hizo,” alisema Dk. Makuwani

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa Sh. bilioni 1.5 katika hospitali za Rufani za Kanda, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na MOI, kuhakikisha wenye mahitaji maalum hasa watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa, wanapata huduma bora na kwa wakati.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Lemeri Mchome, alisema taasisi hiyo inawafikia watoto 500 wenye tatizo hilo kila mwaka, kupitia hospitali za kanda na rufani pia mradi huo utasaidia kuwafikia watoto wengi zaidi, huku takribani 7,000 wakizaliwa na tatizo hilo nchini.

“Nimshukuru Rais Dk. Samia, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuendeleza huduma katika sekta ya afya,  ikiwa ni sehemu ya huduma katika jamii, tunashukuru kwa mageuzi makubwa katika sekta hii ya afya.

Ikumbukwe Rais ameshatoa mchango wa kusaidia matibabu ya watoto 100 wa vichwa vikubwa na mgongo wazi, kwa idadi hiyo itafanya kuwa jumla ya watoto 200 kufikiwa  na huduma  ya matibabu ya vichwa vikubwa na mgongo wazi,” alisema Dk. Mchome.

Machi mwaka huu, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk Julieth Magandi, wakati akipokea vifaa mbalimbali pamoja na kiasi cha pesa za matibabu kutoka kwa  watumishi wanawake wa Bohari ya Dawa (MSD) alisema;

Tatizo la mgongo wazi au vichwa vikubwa, humkumba mtoto yeyote ambaye mama yake hakupata virutubisho alivyotakiwa kuvipata kabla ya kushika ujauzito.

Alisema kwa kawaida virutubisho hivyo vinapatikana katika vyakula vyote vyenye protini na vina uwezo wa kumzuia mama kwa asilimia kubwa asipate changamoto ya kuzaa mtoto mwenye mgongo wazi na kichwa kikubwa.

“Mgongo wazi au (spinal bifida) na vichwa vikubwa ni ulemavu anaozaliwa nao mtoto na akishaupata matibabu yake ni upasuaji wa haraka, ili kuzuia tatizo lisiendelee na katika hatua hii mama anatakiwa kumuwahi pindi anapozaliwa tu afanyiwe matibabu,” alisema.