Airtel kuchochea ukuaji uchumi kidijiti

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 10:25 PM Jun 23 2024
Rais Samia Suluhu Hassan wa kwanza kulia, na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Afrika, Olusegun Ogunsanya kushoto, pamoja na viongozi wengine wakizindua mkongo wa 2Africa.
Picha: Mpigapicha Wetu.
Rais Samia Suluhu Hassan wa kwanza kulia, na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Afrika, Olusegun Ogunsanya kushoto, pamoja na viongozi wengine wakizindua mkongo wa 2Africa.

UCHUMI wa kidijiti unatarajiwa kukuwa zaidi nchini pamoja na kumaliza changamoto ya kukosekana kwa huduma ya intaneti kutokana na kukatika kwa mkongo wa baharini, baada ya Airtel kuanza rasmi kutumia mkongo wa 2Africa unaounganisha Tanzania na mataifa 43 duniani.

Imeelezwa kuwa hatua hiyo italeta mafanikio makubwa katika sekta ya mawasiliano kwakuwa mkongo huo unaunganisha mabara matatu, jambo linalotarajiwa kuleta maendeleo katika kupanua na kuimarisha miundombinu ya kidijitali Tanzania. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Airtel leo, Mkongo huo utaiweka Tanzania katika viwango vya juu vya mabadiliko ya kukua kwa huduma za kidijitali, na kukidhi mahitaji ya uchumi wa nchi, pamoja na kusaidia kuanzishwa kwa vituo vya kuhifadhi kumbukumbu kieletroniki ili kukidhi ongezeko la shughuli za kidijitali nchini.

"Mkongo wa 2Africa sasa umeanza rasmi kuhudumia makampuni ya teknolojia ambayo sasa yanapokea masafa ya uwezo wanaohitaji kupitia kituo cha Airtel Cable Landing Station Kilichozinduliwa siku chache zilizopita na Rais Samia Suluhu Hassan.

"Uzinduzi wa mkongo huo umekuja wakati muafaka, hasa kutokana na kukatika kwa nyaya za mkongo wa mawasiliana unaopita  chini ya bahari hivi karibuni ambazo ziliathiri baadhi ya maeneo ya Afrika Mashariki, ikiwemo  Tanzania," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika uzinduzi huo Rais Samia amesema Mkongo huo unaunga mkono mipango ya Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, ikiwemo ya maabara ya akili mnemba na roboti.

"Miundombinu hii sio tu italeta mapinduzi katika huduma za mawasiliano lakini pia itaharakisha ukuaji wa uchumi kwa kuimarisha muungano na mataifa mengine,” Rais Samia amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Airtel, Dinesh Balsingh, amesema mazingira wezeshi ya serikali pamoja na uwepo wa mfumo bora wa udhibiti ndio sababu zilizowawezesha kuzindua kituo hicho kabla ya nchi nyingine.

“Ujio na uwepo wa mkongo huu wa mawasiliano umefanikiwa kuwa nchini kutokana na maono ya uongozi wa Rais Samia na Waziri wa Habari Mawasiliano na teknolojia ya habari Nape Nnauye. Pia unaifanya Tanzania kuwa kitovu na lango la kusambaza huduma kidijitali kimataifa, kukuza fursa za kiuchumi na maendeleo ya kiteknolojia," amesema Balsingh.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari amesema kuwa mkongo huo utachochea na kuboresha zaidi huduma  bora za intaneti nchini.

“Mkongo  huu mpya utakuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na mahitaji ya huduma za mtandao wa intaneti  nchini, ambazo mahitaji yake yamekuwa yakioongezeka maradufu kila baada ya miaka miwili.

"Nina hakika kuwa teknolojia hii itasaidia utekelezaji wa haraka wa mkakati wetu wa kuhimiza matumizi ya TEHAMA katika sekta zote na kuboresha uchumi wa kidijitali ambao Tanzania inatamani kufikia,” amesema Dk. Bakari.

Waziri Nape amesema uwepo wa mkongo utasaidia kuunganisha nchi kimataifa na kuwepo kwa mifumo ya kibunifu kidijitali ikiwemo kuunganisha mifumo mbalimbali ya serikali kuwa jumuishi. 

Kwamujibu wa makadirio ya 'RTI International' Mkongo wa 2Africa unatarajiwa kuzalisha kati ya dola bilioni 26.4 hadi 36.9 ikiwa ni matokeo ya ukuaji kiuchumi kutokana na huduma zitakazotolewa na mkongo huo barani Afrika ndani ya miaka ya awali.