Makonda: Helikopta itatumika kumchukua mgonjwa na kumkimbiza hospitali

By Beatrice Shayo , Nipashe Jumapili
Published at 10:43 PM Jun 23 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akikagua eneo ambalo litatolewa matibab bure kwa wananchi.
Picha: Beatrice Shayo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akikagua eneo ambalo litatolewa matibab bure kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema kutakuwa na helikopta kwa ajili ya kuwabeba wagonjwa na kuwafikisha hospitali katika kliniki ya utoaji wa huduma bure kwa wananchi.

Kliniki hiyo ambayo ina wataalamu wa kutoa huduma za afya zaidi ya 450 kutoka hospitali mbalimbali nchini wakiwemo madaktari bingwa na taasisi 40 zitaanza kufanya vipimo na matibabu bure kwa wananchi wa jiji la Arusha kwa siku saba kuanzia kesho.

Makonda ameyasema hayo leo wakati akikagua maandalizi hayo kwenye viwanja vya michezo vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo amesema wamejipanga vizuri katika kuwahudumia wananchi.

"Pale kuna helikopta itatumika kumchukua mgonjwa na kumpeleka moja kwa moja hadi hospitali kama itakuwa ni KCMC atapelekwa ama ni Mount Meru atafikishwa au ni hospitali nyingine, hivyo wananchi wajitokeze tuna kila wataalamu watahudumiwa na kupatiwa matibabu bure," amesema Makonda.

Mbali na helikopta hiyo, kuna magari ya kubeba wagonjwa (Ambulance) yamejipanga uwanjani hapo kwa ajili kutoa huduma.

Uwanja huo umezungukwa  na mahema yaliyotengenezwa kwa mfano wa hospitali, hivyo mgonjwa atahudiwa na daktari bila mwananchi kujua kinachoendelea na baada ya kutoka ataingia mwingine kwa kufuata foleni kutokana na viti vilivyopangwa kwa nje.