DC Magoti amuahidi Kunenge kuibadilisha Kisarawe

By Julieth Mkireri , Nipashe Jumapili
Published at 06:33 PM Jun 23 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti.
Picha: Julieth Mkireri
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti.

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti amemuahidi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kuibadilisha wilaya hiyo kimaendeleo kwa kusimamia miradi iliyolengwa kutekelezwa kwa wakati.

Magoti ameyasema hayo aliposhiriki kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani kujadili hoja za mkaguzi wa hesabu za Serikali kilichofanyika mjini humo na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa.


Magoti amesema atahakikisha kila mtendaji anatekeleza majukumu yake sambamba na kusimamia miradi ya maendeleo inakamilike kama ilivyolengwa.

Akiwa katika Baraza hilo Magoti amesema ili kuondoa uzembe kwenye miradi kila mkuu wa idara atakuwa na wajibu wa kusimamia majukumu yake ipasavyo kwa kuwajibika kwenye eneo lake.

" Mkuu wa Mkoa wiki ijayo hapa tutakuwa na kikao na wakuu wa idara na kila mmoja ataeleza mwaka wa fedha unaoisha amefanya nini na mipango yake kwa mwaka ujao ni ipi ," amesema Magoti.

1

Pia amebainisha kwamba anatarajia kufanya ziara hivi karibuni kwenye kata zote za wilaya hiyo, ambapo pia amewapongeza madiwani kwa kazi wanazofanya kwa kushirikiana na Serikali kuondoa Changamoto kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Halmashauri hiyo inatakiwa kuhakikisha inapanga vipaumbele sambamba na kuhakikisha wanafanya matumizi kulingana na bajeti.

Kunenge pia aliwaelekeza Watendaji kuzuia hoja zisitokee sambamba na kumaliza ambazo hazijafungwa kwa kuzingatia maelekezo.
2

Ameagiza kwamba kuanzia sasa kila Mkuu wa idara anatakiwa kuwajibika kuwasilisha hoja zake mwenyewe badala ya kumuachia Mkurugenzi pekee wakati uzalishaji unatoka kwenye idara.

Mkaguzi wa nje Mkoa wa Pwani toka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi CPA Pastory MasaweMkaguzi amesema Halmashauri hiyo inatakiwa kujikita kuzuia kuzalisha hoja mpya na pia kukusanya zaidi mapato na kuwa makini kwenye matumizi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe Beatrice Rest Dominic kwa kushirikiana Watendaji wanaendelea kufunga hoja ambazo zimezslishwa sambamba na kudhibiti uzalishaji wa hoja mpya.
3