Watanzania waaswa kutumia dawa kikamilifu kukabiliana na usugu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:38 PM Jun 16 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akifanya mazungumzo na KIDO—balozi wa kampeini ya Holela-Holela itakukosti jijini Dodoma

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kufuata ushauri wa wataalamu wa afya juu ya matumizi ya dawa ili kukabaliana na usugu.

Hayo amesema mwishoni mwa wiki jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na KIDO ambaye ni Balozi wa Kampeni ya Holela-Holela itakukosti.

“Mtanzania unaweza kufanya mambo machache tu kukabiliana na UVIDA, kama vile; kufuata ushauri wa mtaalamu wa afya kabla ya kutumia dawa, tumia dozi ya dawa kikamilifu kama unavyoshauriwa na mtaalam wa afya, fuata maelekezo ya mtaalam wa mifugo, kilimo juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa mifugo, mimea, na nawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na usafi wa mazingiria kwa ujumla,” amesema Ummy

Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi Mei 25, 2024 na inaratibiwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana Wizara ya Afya, Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Inafadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa--USAID kupitia mradi wa Breakthrough ACTION.

Mwalimu ameelezea msimamo wa Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya UVIDA na ametoa wito kwa jamii kwa kusisitiza Watanzania kutumia dawa kikamilifu kama wanavyoshauriwa wataalam wa afya.