Waonywa kujiingiza mikopo kausha damu

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:04 PM Feb 16 2025
Fedha
PICHA:MTANDAO
Fedha

Serikali imewataka wananchi kuepuka kukopa fedha kwenye taasisi au vikundi vinavyotoa huduma za kifedha bila kusajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka athari zinazoambatana na mikopo umiza.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya  Moshi, Shadrack Mhagama, katika kikao kilichofanyika ofisini kwake alipokutana na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha walioko mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.

Aidha, Mhagama aliwataka wananchi wa halmashauri hiyo hasa watoa huduma za fedha, kuhakikisha wanasajili biashara zao ili kuepuka kuwaumiza wananchi na mikopo kausha damu. 

 Pia aliwataka wananchi waache kukimbilia huduma za haraka ambazo si salama na kuwashauri kuwa kabla ya kuomba mkopo wahakikishe mkopeshaji yuko kihalali kwa mujibu wa sheria.

 “Ni kweli kwa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi tunao watu ambao wanatoa huduma za kifedha lakini hawajasajiliwa. Kwa  kweli tunaweza kusema ni biashara haramu ambayo inafanywa nje ya utaratibu. 

 “Pia imebainika kuwa wananchi wengi wako katika vikundi ambavyo havijasajiliwa rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha ya mwaka 2018. Kwa  hiyo nitoe rai kwa wananchi ni vyema wakawa na mwamko wa kujiunga katika vikundi ambavyo ni rasmi na vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria hiyo,” alisema.

 Mhagama pia alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka  husika ambazo ni pamoja na maafisa maendeleo ya jamii, watakapobaini kuna vikundi vya huduma ndogo ya fedha mitaani vinatoa huduma pasipo kusajiliwa. 

 Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dionensia Mjema, alisema serikali inaendelea na program ya utoaji elimu hapa nchini na kwa sasa ni zamu ya mkoa wa Kilimanjaro.

 Alisema katika programu hiyo, wananchi wamepata elimu namna wanavyoweza kuwa na nidhamu ya kujiwekea akiba lakini pia wamepata uelewa juu ya mikopo umiza ili kuepukana na changamoto hiyo kwa sasa ya mikopo kausha damu.

 Awali, akizungumza katika semina hiyo, mkazi wa Kata ya Uru Mashariki, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi,  Luciana Mushi, alisema ujio wa wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha umewafungua macho kuhusiana na akiba, vyama viwe vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na sehemu salama ya kuweka fedha.

 Philbert Macha ambaye pia ni mwana kikundi kilichoko katika Kata ya Mbokomu, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, alisema kupitia elimu aliyoipata amejifunza mengi na ataenda kuwaelimisha watu wengine maana anaona mikopo mingi inatolewa na watu binafsi na taasisi mbalimbali ambapo wengi wanakopa bila kuwa na malengo.

 Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi za Fedha imetoa elimu ya fedha katika Shule ya Sekondari Mbokomu, vikundi vya kinamama na wajasiriamali wadogo Kata ya Mbokomu na Wanakijiji wa Kata ya Uru Mashariki, Halmashauri ya Wilaya ya  Moshi mkoani Kilimanjaro.