Serikali kuanza mahojiano rasmi na wakimbizi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:59 AM Jun 09 2024
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani) baada ya zoezi la kusaini Nyaraka ya Makubaliano ya Utaratibu wa Urejeaji wa Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa hapa nchini.
Picha: Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani) baada ya zoezi la kusaini Nyaraka ya Makubaliano ya Utaratibu wa Urejeaji wa Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa hapa nchini.

SERIKALI imetangaza kuanza mpango maalumu ifikapo mwakani kuwahoji wakimbizi 158,902 walioko nchini katika kambi mbalimbali zikiwamo za Nduta, Nyarugusu na wanaohifadhiwa katika makazi ya Ulyankulu, Katumba na Mishamo pamoja na vijiji vya mkoa wa Kigoma.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, alisema hayo juzi  baada ya kupokea taarifa ya Kikao cha Wataalamu wa Pande mbili baina ya serikali ya Tanzania na serikali ya Burundi, ikionyesha uwapo wa raia wa Burundi wanaogoma kurejea nchini kwao licha ya amani na utulivu kurejea kwao. 

Kabla ya kikao hicho, serikali zote mbili zilitia saini taarifa ya pamoja ya makubaliano ya urejeaji wa wakimbizi ambapo upande wa Tanzania uliwakilishwa na Waziri Masauni Burundi ikiwakilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia, Theofile Ndarufatiye.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri Masauni aliweka wazi nia ya Tanzania kuendelea kusaidia nchi jirani zinapokuwa katika matatizo ikiwamo matatizo ya vita huku akitoa ahadi ya kuendelea kuzisaidia nchi hizo kupokea na kuhifadhi wakimbizi ambao wanakidhi vigezo vya kuwa wakimbizi.

‘Tumefanya vikao mbalimbali na wenzetu kutoka serikali ya Burundi na wametuhakikishia uwapo wa amani na utulivu nchini Burundi. Lakini  kuna baadhi ya wakimbizi wameonyesha nia ya kutotaka kurejea nyumbani na sisi kama serikali tutaendelea kuwaelimisha umuhimu wa kurejea nyumbani na kuungana na wenzao ili kuweza kuliletea maendeleo taifa lao.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na Mwakilishi wa Serikali ya Burundi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia, Theofile Ndarufatiye(kulia), wakisaini Nyaraka ya Makubaliano ya Utaratibu wa Urejeaji wa Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa hapa nchini.Tukio hilo imefanyika leo mkoani Kigoma.Jumla ya wakimbizi 158,902 wanahifadhiwa hapa nchini.Picha: Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
“Kutokana  na hali hiyo ya kusuasua kwa urejeaji wa wakimbizi hao, sisi kama serikali tumeona ni vyema mapema mwakani kuwahoji wakimbizi kutoka Burundi kwa nini wanasita kurejea nyumbani sambamba na kupima sababu watakazozitoa na kufanya uamuzi sahihi kwa nchi yetu,” alisema.

Naye Ndarufatiye alisema serikali ya Burundi inawahakikishi wananchi wake kuwapo kwa amani huku akiishukuru Serikali ya Tanzania kwa wema na ukarimu wa kuwahifadhi raia wa nchi hiyo kipindi chote ambacho kulikuwepo na hali isiyoridhisha ya amani na usalama nchini humo.

Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Sudi Mwakibasi, alisema utaratibu huo wa kuwahoji utazingatia sheria na kanuni zinazosimamia masuala ya wakimbizi duniani. 

Alisema kazi ya kuwahoji wakimbizi hao itaendeshwa kwa mkimbizi mmoja mmoja na atayethibtika ana haki ya kuendelea kupewa hifadhi ya ukimbizi, ataendelea kuwepo kambini. Alisema atakayethibitika kutokuwa na haki hiyo, atapoteza hadhi ya ukimbizi na atakabidhiwa barua ya kuondoka nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na Mwakilishi wa Serikali ya Burundi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia, Theofile Ndarufatiye(kulia), wakibadilishana Nyaraka ya Makubaliano ya Utaratibu wa Urejeaji wa Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa hapa nchini.Tukio hilo imefanyika leo mkoani Kigoma.Jumla ya wakimbizi 158,902 wanahifadhiwa hapa nchini.Picha:Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.