Sababu ongezeko upasuaji wa nyonga, magoti yatajwa

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 12:56 PM Feb 16 2025
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko
Picha: Mtandao
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, imesema idadi kubwa ya wanaofanyiwa upandikizaji wa nyonga na magoti, ni wenye uzito kupindukia hasa wanawake wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea.

Imesema tangu kuanza kwa huduma ya upandikizaji mwaka 2023, waliokwishapandikizwa nyonga na magoti ni 263 huku baadhi yao chanzo kikiwa ajali, umri, jinsi (gender) na hasa wenye uzito mkubwa usiolingana na kimo.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko, aliyasema haya jana, Dar es Salaam, akieleza kuhusu kambi maalum ya upasuaji wa marejeo wa kupandikiza nyonga na magoti. Kambi hiyo ya siku 10 itafanyika kuanzia Februari 26 hadi Machi 7, mwaka huu.

“Hospitali imeendelea kujikita katika huduma za kibingwa na ubingwa bobezi na katika kuhakikisha huduma hizi zinakuwa endelevu na kuhakikisha Watanzania wananufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya afya tumeandaa kambi maalum.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila, Dk. Godlove Mfuko
“Upasuaji wa marejeo (revision) wa kupandikiza nyonga na magoti, itafanyika kwa kushirikiana na Bingwa Mbobezi wa Upandikizaji wa Viungo kutoka China, Dk. Tian Hua, ambaye amebobea katika eneo hilo,” alisema.

Dk. Mfuko alisema ni mara ya kwanza katika hospitali za umma hapa nchini kufanya  huduma hiyo ya upasuaji wa marejeo wa nyonga na magoti ambayo kwenye kambi itahudumia wagonjwa 20 hadi 30.

“Huduma kama hii ikifanyika nje ni takribani Sh. milioni 30 lakini hapa nchini ni wastani wa Sh. milioni 15 sababu kuu ni vifaa vya upandikizaji ni ghali. Hivyo ni vyema mtu akatunza uzito wake sahihi.

“Kufanyika kwa kambi hii kunatokana na uhitaji wa watu wengi wanaokuja kutafuta huduma hiyo hospitalini hapa na kutofanikiwa. Uongozi ukaona ipo haja ya kuwapunguzia usumbufu wa maumivu na gharama za kutafuta huduma hizi nje ya nchi,” alisema. 

Aliongeza kuwa: “Serikali imeendelea kuwajengea uwezo wataalam wa ndani, ili kufanya huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kama hizi, sasa ni wajibu wetu sisi, awali upasuaji huu ulikuwa haufanyiki nchini kutokana na upatikanaji wa nyonga, magoti bandia maalum, kwa ajili ya upasuaji wa marejeo pamoja na utaalam.”

Bingwa wa Nyonga na Magoti kutoka MNH-Mloganzila, Dk. Abubakar Hamis, alisema kutokana na waliofanyiwa huduma hiyo kufanyika wakati teknolojia ikiwa duni, ndio sababu ya kufanyiwa upasuaji wa marejeo.

“Baada ya miaka kadhaa kupita vyuma hulegea, husagika katika maeneo vilikowekwa. Maambukizi pia ni sababu ya upasuaji wa marejeo, kidonda kinaweza kupata bakteria baada ya upasuaji.

“Mvunjiko palipowekwa kiungo au palipounganishwa ni sababu ya marejeo. Lakini zaidi ni uzito, uzito husababisha nyonga, magoti kusagika paliporekebishwa,” alisema.