Neema makandarasi, wazabuni nyongeza bajeti

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 12:33 PM Feb 16 2025
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba,
Picha: Mtandao
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba,

BUNGE limepitisha ongezeko la bajeti ya serikali ya mwaka 2024/25 kwa Sh. bilioni 945.7 na kufikia Sh. trilioni 50.29 kutoka Sh. trilioni 49.34 iliyoidhinishwa awali.

Kati ya fedha hizo za nyongeza, Sh. bilioni 325.9 zitatumika kulipa malipo ya madeni ya watumishi, wakandarasi na wazabuni wa ndani na ujenzi wa miundombinu ya serikali katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma. 

Akiwasilisha bungeni jana mapendekezo ya nyongeza ya bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema fedha hizo zimeelekezwa kutekeleza shughuli za sekta za elimu na afya, taasisi za utalii na utekelezaji wa programu mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pia alisema mgawanyo wa fedha hizo umezingatia maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi kwa kuhakikisha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ya amali ni kwa vitendo.

“Aidha, kupitia fedha hizi, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa utoaji na upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii ni endelevu.  

Vilevile, mgawanyo wa fedha hizo umezingatia mapendekezo ya sekta tajwa, makubaliano kati ya Serikali na washirika hao wa maendeleo pamoja na ushauri wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti,” alisema.

Waziri alisema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetengewa Sh. bilioni 131.4 kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya
 mtaala mpya wa sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari za amali, upatikanaji wa vifaa na walimu.

Pia alisema fedha hizo zitagharamia ukamilishaji wa ujenzi wa vyuo vya VETA, ujenzi wa maktaba ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), ujenzi wa miundombinu ya Chuo cha Nelson Mandela - Arusha, ujenzi wa jengo la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mkoani Mwanza na ujenzi wa jengo la maktaba  Mwanza.

Kadhalika, alisema Wizara ya Afya imetengewa Sh. bilioni 53.7 kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.

“Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Sh. bilioni 173.7 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia miundombinu katika sekta ya afya na elimu pamoja na kuiwezesha TARURA (Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini)  kukarabati miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa na mvua ya masika, hivyo kuweza kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

 Pia, alisema Wizara ya Maliasili na Utalii imetengewa Sh. bilioni 260.7 kwa ajili ya kugharamia uendeshaji, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika hifadhi za taasisi za utalii za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Awali, alifafanua kuwa fedha hizo zimetokana na Desemba, 2024, Serikali ilikuwa imepokea Sh. Bilioni 460 kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Sh. bilioni 130 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambazo hazikuwa
 sehemu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

“Fedha za AfDB zilikuwa zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2023/24 zikachelewa kupatikana kwa wakati na zikaingia Mfuko Mkuu wa Serikali mwaka 2024/25,” alisema.

Alisema katika nusu ya pili ya mwaka 2024/25, serikali inatarajia kupokea zaidi ya sh. bilioni 356 kutoka IMF ambazo nazo si sehemu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

“Fedha hizi kutoka IMF hazikujumuishwa kwenye bajeti ya mwaka 2024/25 kwa kuwa majadiliano yake yalikamilika katika kipindi ambacho mapendekezo ya bajeti ya serikali yalikuwa yameshawasilishwa bungeni na
 kuidhinishwa,” alisema.

Alisema kwa mwaka 2024/25 serikali itapata ziada ya Sh. bilioni 945.7 ambayo si sehemu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge na hivyo imewasilisha mapendekezo ya nyongeza hiyo ili kuidhinishwa na kutimiza matakwa ya ibara 137(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa= Tanzania na kifungu cha 43 cha Sheria ya Bajeti Sura ya 439.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Twaha Mpembenwe, alisema kwa kuwa Serikali ilikwisha chukua orodha ya vituo vya afya vya kimkakati vinavyotakiwa kujengwa kila jimbo kutoka kwa Wabunge, orodha hiyo iheshimiwe na ndio itumike katika ujenzi.

“Kamati ya Bajeti katika Bunge la mwezi Machi 2025, itafanya ufuatiliaji wa utolewaji wa fedha na ujenzi wa vituo hivyo vya afya na endapo itaonekana orodha imekiukwa itapendekeza kwa Bunge hatua stahiki za kuchukua kwa wahusika,” alisema.

 Kadhalika, alisema Ofisi ya Rais - TAMISEMI mwaka 2024 ilikamilisha tathmini ya mahitaji ya fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma yote nchini na kubaini kwamba zilihitajika Sh. bilioni 228.24. Hivyo, kiwango kinachopendekezwa Sh.bilioni 71 kitapungunguza mzigo wa ujenzi wa maboma kwa walau asilimia 31.1.

“Kamati inatoa rai kwa Serikali kwamba mgawanyo wa fedha hizi uzingatie mahitaji, hali ya uchumi ya Halmashauri, uwezo wa kimapato na mgawanyo linganifu. Kamati haitarajii kuona kuna majimbo yananufaika kuliko mengine bila kuzingatia viashiria hivyo,” alisema.

Aidha, alisema kamati inaitaka serikali kuwasilisha orodha ya maboma yatakayokamilishwa mapema iwezekanavyo ili Wabunge wapate fursa ya kuyahakiki.

Pamoja na hayo, alisema uzoefu unaonyesha zinapopatikana fedha na mwaka wa fedha unaenda kuisha masuala mawili hujitokeza ama kuwe na matumizi mabaya au fedha zirudishwe hazina kutokana na fungu husika kushindwa kutumia hadi mwisho wa mwaka.

“Kamati inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya ukaguzi wa wakati yaani Real Time Audit ya Fedha hizi ili kuzuia ubadhirifu na inatoa rai kwa maofisa masuuli wote kufuata kanuni za Sheria ya Bajeti Sura ya 439 ambazo zinawataka kumjulisha mlipaji mkuu wa serikali kuhusu fedha za maendeleo ambazo wanaomba kuvuka nazo mwaka siku 30 kabla ya tarehe ya mwisho ya kutekeleza Bajeti ya mwaka husika ili wazitumie katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha unaofuata,”alisema.

Katika hatua nyingine, Bunge limepitisha muswada wa sheria ya kuidhinisha matumizi ya nyongeza ya serikali kwa mwaka 2024/25.