Mwandishi akamatwa kisa kupiga picha gari la mafuta

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:13 AM Jun 16 2024
Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton.
Picha: Mtandao
Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton.

NAIBU Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton, amekamatwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, kwa zaidi ya saa mbili na nusu kwa kupiga picha lori lililopinduka.

Akiwa safarini eneo la mji wa Same, Manyerere alikuta lori lililobeba mafuta ya kula likiwa limepinduka  na wananchi wanaokadiriwa kuwa hadi 200 wamelivamia wakiwa na ndoo na madumu yaliyoashiria kuchota mafuta hayo.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Manyerere alisema baada ya kukuta tukio hilo saa 4:00 asubuhi alipiga picha na akiwa katika kufanya hivyo, ghafla polisi wasiozidi saba walimvamia na kuanza kumghasi kisha kuchukua simu aliyokuwa akiitumia kupiga picha na kufuta kila alichorekodi.

“Ilikuwa asubuhi majira ya saa 4:00, nilikuwa nje kidogo ya mji wa Same kama kilomita 15 hivi. Nilifika pale nikaona kuna ajali, nikaegesha gari pembeni nikashuka nikaanza kuzungumza na askari wakasema ni ajali ya semi trailer lilikuwa limebeba mafuta ya kula.

“Ajali ilitokea usiku kwahiyo, wananchi wakaingia pale wakaanza kumpiga dereva na wakaanza kufanya vurugu na kupora mafuta.

“Wamepora (mafuta), polisi walivyofika pale wakaanza kuzuia. Kwa hiyo mimi nilipofika pale nikakuta kundi kubwa la wananchi wako takribani kama 150 au 200 hivi, wako upande wa pili wa barabara wana ndoo na vyombo vya kuteka yale mafuta,” anasimulia Manyerere.

Manyarere alisema walipomkamkata, walimpeleka hadi Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Same, kwa lengo la kumhoji lakini aliachiwa baadaye kwa amri ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Simon Maigwa.

Alisema msukumo alioupata pale ni kwamba imekuwaje mbona kwenye ajali ndiyo watu wanataka wanufaike badala ya kusaidia.

"Kwa hiyo nikapiga picha wale wananchi wakiwa na madumu yao na pembeni gari likiwa limelala. Nikapiga picha kama nne za wananchi na lile lori. Polisi mmoja akaniuliza kwa nini unapiga picha? Nikamjibu ndugu yangu tuko kazini.

“Akauliza tena wewe nani? nikamwambia mimi mwandishi wa habari na Mhariri wa Gazeti la Jamhuri. Akauliza tena kwa nini unapiga picha bila kibali? Nikamwambia ninapiga picha tukio la barabarani, lakini kama ingekuwa ni Kituo cha Polisi, sawa!

“Wakanikaba pale, walikuwa kama sita au saba hivi. wakaninyang'anya  simu, akaja mkubwa wao ana nyota tatu akaamuru niingizwe kwenye gari lao lakini nikagoma. “Tukaenda kituo cha Same nikaa pale kama saa mbili au tatu hivi wakaniachia baada ya mkuu wa kituo kunisikiliza na kuona si kosa,” alisimulia.

POLISI WAFUNGUKA

Kamanda Maigwa alisema jeshi hilo lililazimika kutumia nguvu kwa kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya zaidi ya wananchi 600 waliokuwa wamevamia lori lililokuwa limebeba mafuta ya kula aina ya 'Korie' lililopata ajali eneo la Njoro.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi na lori lenye namba za usajili T 783 CTC aina ya HOWO na trela lake namba T 889 CSK likitokea Dar es Salaam kwenda Arusha, liliacha njia na kupinduka, hivyo kusababisha uharibifu huo.

Kamanda Maigwa alisema askari mmoja alijeruhiwa na kitu butu (jiwe) kichwani na mwananchi aliyekuwa akipinga amri ya kuondolewa eneo hilo.

Wakati huo huo, Mwandishi wa Habari na Mmiliki wa Dima Tv, Dina Maningo, aliyeshikiliwa kwa siku mbili na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, aliachiwa kwa dhamana jana jioni.

Dina alikamatwa Alhamisi  wiki hii kwa tuhuma za kutumia nyaraka za siri za Jeshi la Polisi za kesi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Yahaya Nawanda, anayedaiwa kumlawiti mwanafunzi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi  wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko, aliiambia Nipashe jana kuwa mwandishi huyo ameachiwa kwa dhamana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Wilboard Mutafungwa, alisema wanamshikilia Nawanda kwa tuhuma za kumlawiti binti huyo (21) Juni 2, mwaka huu, usiku katika eneo la baa ya The CASK, viwanja vya jengo la Rock City Mall.

Alisema mahojiano  yanaendelea kwa kushirikisha taasisi zingine na wakikamilisha watapeleka Ofisi ya Mashitaka ya Taifa.

Kamanda Mutafungwa alisema mtuhumiwa anashitakiwa na Jamhuri na mlalamikaji ni shahidi katika kesi hiyo, huku akikanusha nyaraka zinazosambaa mitandaoni siyo sehemu ya uchunguzi wao.

 Alisema gari linalodaiwa kufanyika kitendo hicho wameshalikamata na wanaendelea na mawasiliano na watu wa mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kulipeleka Mwanza. Pia  aliwataka wanaosambaza habari hizo bila kujali utu wa binti huyo, watambue wako kinyume na sheria ya kulinda utu wa mtu.