Mageuzi yapaisha sekta ya utalii

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe Jumapili
Published at 08:48 AM Jun 09 2024
news
Picha: Mtandao
Waziri wa Malisili na Utalii, Angellah Kairuki, akiwa kwenye gari la kubeba watalii, (kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

WAZIRI wa Malisili na Utalii, Angellah Kairuki, amesema maboresho yaliyofanywa na serikali katika sekta ya utalii yamechangia ongezeko kubwa la watalii wa nje ya nchi na ndani wanaotembelea vivutio vya utalii nchini.

Aidha, amewapongeza wadau binafsi wa sekta ya utalii ambao wanafanya kazi kubwa ya kutangaza vivutio vya utalii nchini, wakiwamo Karibu Kili Fair ambao kila mwaka wanafanya maonyesho ya kimataifa ya utalii yanayowakutanisha watoa huduma na wanunuzi katika sekta hiyo. 

Waziri Kairuki alisema hayo jana wakati akifungua maonyesho ya Karibu Kili Fair (KKF) ambayo  yameshirikisha zaidi ya wanunuzi 600 wa bidhaa mbalimbali za utalii kutoka nchi 42 duniani na wadau wa utalii 468 kutoka nchi 37.  

"Mazingira bora ya biashara  kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi yamekuwa na tija kubwa katika sekta ya utalii tumeona idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi wakiongezeka kila siku.Nataka niwahakikishie kwamba serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hii muhimu kwa taifa,"alisema Waziri Kairuki na kuongeza kuwa; 

"Sekta ya utalii hapa nchini inachangia pato la taifa kwa asilimia 17.2 huku ikichangia asilimia 25 ya fedha za kigeni lakini mafanikio yote haya yanatokana na  ushirikiano mzuri wa  serikali na sekta binafsi," alisema. 

Waziri Kairuki alisema  maonyesho hayo ya kimataifa yana tija kubwa kwa kuwa yanawakutanisha watoa huduma za utalii nchini na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali za utalii ikwemo safari na hoteli. 

"Ni imani yangu kwamba maonesho haya yatawakutanisha wanunuzi na wauzaji wa bidhaa mbalimbali za utalii na yatatoa fursa ya kufanya biashara mbeleni ambayo yatakua na tija kwa taifa," alisema. 

Naye Mkurugenzi wa Karibu Kili Fair, Dominic Shoo,  alisema amepokea ushauri uliotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuwa anatambua mchango wao mkubwa katika kukuza sekta hiyo muhimu. 

Shoo alisema maonyesho hayo yanawawezesha kukua na kufikia viwango vya kimataifa, wanaomba wadau wa utalii kuendelea kushiriki ili kumuunga mkono Rais  Samia Suluhu  Hassan, katika juhudi za kitangaza vivutio vya utalii, katika kufikia masoko ya utalii ulimwenguni.

Mkurugenzi huyo aliomba mawakala wa utalii nchini kuendelea kuunga mkono kwa kushiriki maonyesho hayo ili kuongeza idadi6 ya watalii iweze kufikia milioni tano  ifikapo mwaka 2025. 

"Lakini naomba Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) tuendelee kuahirikiana katika kutangaza vivutio mbalimbali vinavyopatikana hapa nchini,"alisema.  

Mmoja wa waonyeshaji wa bidhaa wa sekta ya utalii kutoka kampuni ya Serengeti Balloon Safaris, Gloria Kanza,  alisema maonyesho hayo yanatija kubwa katika kukuza sekta ya utalii na uchumi nchini, ambapo wamekutana na wanunuzi mbalimbali wa kimataifa ambao wameonyesha nia ya kuleta watalii nchini.