Muhoozi atishia kushambulia Mji wa Bunia huko DRC

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 01:23 PM Feb 16 2025
Mkuu wa vikosi vya Ulinzi vya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Picha: Mtandao
Mkuu wa vikosi vya Ulinzi vya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema Uganda inatoa saa 24 vikosi vyote vilivyopo katika Mji wa Bunia Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lasivyo Jeshi lake litashambulia Mji huo.

Kainerugaba ametoa kauli hiyo Februari 15 katika mtandao wake wa X. Huku akielezwa  kuwa na historia ya kuchapisha maoni ya uchochezi kuhusu sera za kigeni mara kwa mara.

Alisema ana mamlaka ya Rais Yoweri Museveni, ambaye pia ni babake ambako hata hivyo, alipotafutwa Msemaji wa jeshi la Uganda alisema hawezi kuzungumzia suala hilo.

Kabla ya kuchapisha ujumbe huo,  Kainerugaba alikuwa alieleza bila kutoa ushahidi, kwamba watu kutoka kabila la Bahima walikuwa wakiuawa huko DRC 

"Watu wangu, Bahima wanashambuliwa. Hiyo ni hali ya hatari sana kwa wale wanaowashambulia watu wangu. Hakuna mtu katika dunia hii anayeweza kuwaua watu wangu na kufikiri hatateseka kwa ajili yake!,"aliandika.

Aliendelea kuwa "Bunia hivi karibuni itakuwa mikononi mwa UPDF (Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda)".

Waziri Mkuu wa Kongo Judith Suminwa aliambia Reuters kando ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika siku ya Jumamosi kwamba serikali yake "haina maoni ya kutoa" kuhusu matamshi ya Kainerugaba.

Tishio hilo kutoka kwa afisa mkuu wa jeshi la Uganda, ambaye mara kadhaa ametajwa kuwa mrithi wa Museveni, limezua hofu kwamba mzozo kati ya vikosi vya Kongo na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda unaweza kuzuka na kusababisha vita vya kikanda.

Siku ya Ijumaa, kiongozi wa M23 alisema waasi hao waliingia Bukavu, mji wa pili kwa ukubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya kutekwa kwa Goma, jiji kubwa zaidi, mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kainerugaba ameonekana kuwa akimuunga mkono hadharani Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye amekanusha madai kwamba wanajeshi wa Rwanda wanapigana pamoja na M23.

Mnamo 2022, Kainerugaba aliitaja M23 kama "ndugu zetu" wanaopigania haki za Watutsi nchini Kongo.

Waangalizi walisema machapisho hayo yanalenga kutuma ujumbe kuhusu maslahi ya kiuchumi na kisiasa ya Uganda katika jimbo la Ituri nchini Kongo, ambalo Bunia ni mji mkuu wake.