Waziri ataja vikwazo maendeleo uchumi wa buluu

By Paul Mabeja , Nipashe Jumapili
Published at 12:48 PM Feb 16 2025
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad  Masauni.
PICHA:MTANDAO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yusuf Masauni, amesema licha ya uwapo wa sera, sheria, na miongozo, bado kuna changamoto mtambuka zinazochangia taifa kutonufaika ipasavyo na rasilimali za uchumi wa buluu.

Masauni alisema hayo juzi jijini hapa, wakati wa kikao cha mawaziri cha kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za uchumi wa buluu nchini kwa mwaka 2024/25 na 2025/26.

 Alisema uchumi wa buluu ni dhana inayochagiza ukuaji wa uchumi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na ushirikishwaji wa jamii.

 “Shughuli za uchumi wa buluu nchini zinatekelezwa kwa sera, sheria, miongozo, mikakati na mipango ya kisekta ikiwemo, uvuvi, nishati, uchukuzi, maliasili na utalii, maji, umwagiliaji, viwanda na biashara, uhifadhi wa mazingira, madini na uwekezaji.

 “Pamoja na uwepo wa sera na sheria hizo, kumekuwepo na changamoto mtambuka zinazochangia Taifa kutonufaika ipasavyo na rasilimali za uchumi wa buluu zikiwamo kukosekana kwa mfumo jumuishi wa kitaasisi wa uratibu wa shughuli za uchumi wa buluu,” alisema.

 Aliitaja changamoto zingine kuwa ni ni kukosekana kwa mpango wa matumizi wa maeneo ya maji, uwekezaji usio wa kimkakati na fungamanishi katika matumizi ya rasilimali za uchumi wa buluu na uhaba wa utafiti na ujuzi katika matumizi ya rasilimali za uchumi wa buluu. 

 Alisema kutokana na changamoto hizo  serikali iliandaa na kupitisha Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya Mwaka 2024 na mkakati wake wa utekelezaji wa mwaka (2024-2034) iliyozinduliwa Juni 5, 2024.  

 “Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya Mwaka 2024 imezingatia maeneo muhimu ambayo ni uratibu wa shughuli za uchumi wa buluu ili kuwa na mfumo jumuishi wa uratibu miongoni mwa wadau wanaosimamia na kutekeleza shughuli za uchumi wa buluu nchini.

 “Pia matumizi ya maeneo ya maji ili kuwezesha nchi kunufaika ipasavyo na fursa za uchumi wa buluu kwa kuzingatia mahitaji ya shughuli za kiuchumi, kijamii na uhifadhi wa mifumo ikolojia na mazingira na usimamizi katika eneo la ukanda maalumu wa uchumi wa bahari na bahari kuu ili kuimarisha uratibu wa rasilimali zote katika eneo la ukanda maalumu wa uchumi wa bahari na bahari kuu,” alisema 

 Pia alisema Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwa msimamizi mkuu wa masuala ya uchumi wa buluu nchini, imepewa jukumu la kuratibu utekelezaji wa shughuli za uchumi wa buluu Tanzania Bara kwa kuratibu, kufuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji shughuli zote.

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Ashatu Kijaji, alisema lengo ni wanachi kunufaika na rasilimali zilizopo na alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha mwelekeo wa nini kifanyike katika eneo hilo.

 Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa mwaka 2023, sekta ya uvuvi imeendelea kukua na kutoa mchango mkubwa katika ajira na usalama wa chakula.

 Pia, uzalishaji wa mazao ya uvuvi unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 473,592 hadi tani 639,092, sawa na ongezeko la asilimia 34.9 kwa mwaka 2024.

 Hata hivyo, Tanzania, uchumi wa buluu unajumuisha shughuli za kiuchumi zilizoendelevu zinazohusiana na bahari, maziwa, mito, mabwawa, maeneo oevu na maji chini ya ardhi kwa manufaa ya jamii bila kuathiri mazingira.