CCM yageukia ufufuaji viwanda Tanga

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 09:06 AM Jun 09 2024
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akifanya ziara katika kiwanda cha uzalishaji wa nyaya za umeme cha Tanga Cable Ltd.
Picha: Romana Mallya
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akifanya ziara katika kiwanda cha uzalishaji wa nyaya za umeme cha Tanga Cable Ltd.

WAKATI serikali ikianika mikakati yake ya kuvifufua viwanda vilivyokufa mkoani Tanga kwa kuwaita waliovinunua ili kuvifufua, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uwekezaji huo utajenga uchumi imara na nchi kwa kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

Akizindua kiwanda cha kuzalisha nyaya za umeme cha Tanga Cable mkoani hapa kwa ajili ya kuunganisha umeme vijijini ukanda wa Kaskazini-Mashariki, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alitaka bidhaa za ndani ziungwe mkono.

Balozi Nchimbi alitoa wito kwa taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini kupitia viwanda vilivyopo na vinavyoanzishwa. Alisema wanahitaji viwanda vya ndani si kwa ajili ya mapambo bali kujenga uchumi.

Balozi Nchimbi alitaka jitihada zinazofanywa na wazawa zisipotee bure hivyo, waungwe mkono kwa bidhaa zao kununuliwa.

Alisema uzinduzi wa kiwanda hicho ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwamba  wanatambua kwamba hakutakuwa na mafanikio ya kweli kama sekta binafsi haitashiriki katika ujenzi wa taifa.

Balozi Nchimbi alisema wanapata faraja kuona wazawa wanachukua hatua na kuanzisha viwanda.

“Tunayo changamoto kubwa ya uagizaji wa bidhaa nyingi nje. Tungependa  tufike mahali tujitegemee katika uzalishaji wa bidhaa zetu sisi wenyewe ndani, tuwe na viwanda vya kutosha ambavyo vitasaidia kwanza, kubadilisha urari wa kibiashara.

“Kwamba tuwe na uwezo wa kuuza zaidi ya tunavyonunua ili kujipatia fedha za kigeni za kutosha na kuendesha mambo yetu mbalimbali ya uchumi wa nchi,” alisema.

Pia alisema kwa kuwa na viwanda kunawezesha upatikanaji wa ajira za kutosha kwa wananchi na kupunguza gharama za usafirishaji ambazo ni kubwa wanapoagiza bidhaa nje.

“Tunawapa shime watanzania wote wenye nguvu za kuwekeza waige mfano wenu na wa wengine waliofanya jambo kama hili ili kujenga viwanda vidogo na vikubwa,” alisema na kubainisha kuwa hali hiyo itasaidia kujenga na kuimarisha uchumi wa nchi.

Aliwahakikishia wawekezaji hao kwamba CCM itaendelea kusimamia sera yake ya kuhakikisha sekta binafsi inafanyiwa mazingira ya uwezeshaji ili maendeleo endelevu kupatikana kwa urahisi, lakini kasi ya kukua kwa uchumi wa nchi iwe kubwa zaidi kuliko hivi sasa.

“Nitoe wito kwa taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi kuona jitihada zinazofanywa na wafanyabiashara wazawa zisipotee bure kwa kadri inavyowezekana tutumie bidhaa za ndani na hasa tukishajiridhisha ubora wake.

“Chama Cha Mapinduzi kitatumia nafasi hii kusisisitiza mara kwa mara kwamba, tunahitaji viwanda vya ndani si kwa ajili ya mapambo, tunavihitaji ili vishiriki kujenga uchumi wa nchi yetu,” alisema.

Mkurugenzi wa Tanga Cable, Murtaza Dossaji,  alisema kiwanda hicho ni kwa ajili ya kuzalisha nyaya za umeme kwa ajili ya kupeleka na kuunganisha umeme vijijini.

Alisema ni kiwanda pekee katika kanda ya Kaskazini-Mashariki kinachozalisha nyaya hizo za umeme, kilichoanzishwa na wazawa, wakiwekeza zaidi ya Sh. bilioni moja na kinatarajia kuajiri zaidi ya wafanyakazi 50.

“Lengo la kiwanda ni kuboresha sekta ya umeme Tanzania kwa ujumla, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kanda ya Kaskazini na makandarasi wa REA  (Wakala wa Nishati Vijijini) ambao wamepata kazi katika kanda hii watanufaika kwa kupata nyaya kwa bei nafuu na usafirishaji wake utapungua kwa kuwa zipo ukanda huu.,’ alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, alisema Tanga ni mkoa uliokuwa ukisifika kwa viwanda, lakini vingi vimekufa na vilivyobinafsishwa vingi vimenunuliwa na kufanywa magofu.

“Hivi vinavyochipuka na kumea wanataka viendelee kushamiri ili kuwa na uchumi mkubwa. Maelekezo ya chama ni kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa vinafufuka na tayari tumepanga mkakati wa kuwaita walionunua viwanda hivyo vifufuliwe.

“Pia kushawishi wawekezaji wapya kuja kufungua viwanda kwa sasa tuna karibu viwanda vitatu vya saruji na hivyo, tunategemea tuendelee kuwa navyo vingi katika sekta ya uchumi wa buluu na sekta ya kilimo katika kuongeza thamani , madini ujenzi na umeme ikiwamo hiki cha Tanga Cable,” alisema.