Wazazi wasiache kutenga bajeti ya taulo za kike kwa mabinti zao

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 10:42 AM Jun 07 2024
Taulo za kike.
Picha: Mtandao
Taulo za kike.

KILA mzazi wenye mtoto wa kike ambaye kapevuka, ana wajibu wa kumtengea bajeti ya taulo ngumu kila mwezi, ili kumsaidia katika usalama wa maisha hayo.

Hedhi salama inamsaidia mtoto kuwa huru na kama ni mwanafunzi, anapofika hatua hiyo anaishi pasipo shaka yoyote, juu ya usalama wake. 

Kwa baadhi ya familia, suala la hedhi salama kwa mtoto wa kike, wanaona suala hilo linasimamiwa na mzazi mmoja ambaye ñi mama na sio baba.

Kiuhalisia, suala la hedhi salama linatakiwa kuzingatiwa na wazazi wote katika kumtengea mtoto bajeti yake kila mwezi. 

Ni lazima lizingatiwe ili kumwezesha mtoto wa kike kuyafikia malengo yake. 

Wapo wanafunzi wa kike wanashindwa kuyafikia malengo yao kutoka na kukosa vifaa vya kujistiri wakati wa hedhi. 

Wapo wanakuwa na vifaa vya kujistiri, lakini changamoto nyingine inakuja pale mwanafunzi anapokosa chumba cha kujisitiri. 

Hayo yote yakifanyiwa kazi, maana yake,  yatamsaidia mtoto wa kike kuwa katika hedhi salama kila mwezi. Hivyo, wazazi na walezi  nchini wanatatakiwa kuhakikisha wanawawezesha watoto wa kike kila mwezi kupata vifaa vyao vya kujilinda na kuwa na hedhi salama katika muda husika. 

Ni sauti inayotolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, katika kilele cha maadhimisho ya jumla ya Hedhi Salama Duniani, kitaifa yakiidhimishwa jijini Arusha. 

"Wazazi mara nyingi tumekuwa tukitenga bajeti ya kununua vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi majumbani kwetu. 

“Lakini, eneo hili la kununua pedi ‘taulo za kike’ mara nyingi tunakuwa tunalisahau, niwaombe wazazi na walezi wote tutenge bajeti ya kila mwezi kwa ajili ya kuwezesha hawa mabinti zetu waweze kuwa na uhakika wa kuwa na taulo za kike na kufikia malengo ya hedhi salama,” anasema. 

Anaongeza kuwa, serikali imekuwa ikihimiza uwekezaji wa uzalishaji bidhaa za hedhi nchini ili ziweze kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu.  

Pia, katika hilo anapongeza mchango wa wadau wa sekta tajwa, katika kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa taulo hizo. 

"Napenda kutoa pongezi kwa Kiwanda cha A-Z kilichopo hapa Arusha, kwa kuanzisha uzalishaji wa bidhaa hizi muhimu nchini, ambayo kwa sasa wanazalisha taulo za kike zitakazoweza kutumika kwa muda mrefu," anasema. 

Anafafanua kuwa, pia wanakaribisha  wazalishaji wengine kujitokeza kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa za hedhi, ili ziweze kupatikana kwa wingi na kwa gharama nafuu nchini.  

Akisoma taarifa ya Jukwaa la Hedhi Salama nchini, Mariam Mashimba, Mwenyekiti wa jukwaa hilo anasema hivi sasa watumiaji wengi katika shule wanapendelea taulo za kufua.  

"Wakati wa utafiti asilimia 75 ya wanafunzi waliohojiwa katika baadhi ya shule za sekondari na msingi ndani ya mikoa 22, ambako utafiti ulifanyika, walionyesha kupendelea zaidi taulo za kufua kwani huokoa uchumi wa wazazi wao na kutunza mazingira, pia huondokana na adha ya kukosa mahali pa kutupa pindi wanapomaliza kutumia," anasema. 

Mwakilishi wa Mkoa wa Arusha, Dk. Omary Chande, akitoa salamu za mkoa, anasema mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa iliyopokea fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza afua za afya. 

"Katika mwaka wa fedha 2023/24 mkoa ulipokea zaidi ya Sh. bilioni 33.2 za uboreshaji wa miundombinu ikiwapo Hospitali ya Mkoa, wilaya na vituo vya afya," anasema.